Familia za abiria wa ndege iliyotoweka zasubiri habari
WAIKWA MAINA, VALENTINE OBARA na STELLA CHERONO
FAMILIA za watu kumi waliohusika kwenye ndege inayoaminika kutoweka katika Msitu wa Aberdare mnamo Jumanne, zilikuwa na matumaini ya kupata jamaa zao wakiwa hai, zaidi ya saa 48 baada ya ndege hiyo kutoweka angani.
Waliokuwa kwenye ndege hiyo ni marubani Barbra Wangeci Kamau na Jean Mureithi. Abiria walitambuliwa kama Ahmed Ali Abdi, Karaba Sailah Waweru Muiga, Khetia Kishani, Matakasakaraia Thamani, Matakatekei Paula, Ngugi George Kinyua, Pinuertorn Ronald and Wafula Robinson.
Ndege hiyo iliyokuwa imetoka Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia saa kumi jioni kuelekea Nairobi, ilitoweka saa 11:20 jioni, na kufikia wakati kuchapisha gazeti ilikuwa haijapatikana.
Maafisa wa vikosi vilivyohusika katika kuitafuta walisema hali mbaya ya hewa ilitatiza shughuli hiyo na kupelekea kusitishwa dakika chache kabla saa kumi na moja jioni jana.
Wakazi wa eneo la Njabini, ambako ndege hiyo ilitoweka, walisema hali ya hewa ilikuwa mbaya sana Jumanne jioni.
“Mvua kubwa ilikuwa inanyesha na kulikuwa na ukungu tulipokuwa tukitoka kazini Jumanne jioni, wakati ambapo inasemekana ndege ilitoweka,” akasema mkazi, Bw Job Wambugu.
Shirika la ndege la Fly-Sax linalomiliki ndege hiyo, lilifungua kituo cha kutoa habari na ushauri nasaha kwa familia za wasafiri na marubani katika Hoteli ya Weston, jijini Nairobi.
Ingawa helikopta kadhaa zilitumwa Njabini kusaidia katika shughuli ya uokoaji, ilikuwa vigumu kwani marubani hawangeweza kuona vyema kwenye ukungu.
Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Majanga Kitaifa (NDMU) Pius Masai, alisema ilikuwa ni muhimu kuhakikishia waokoaji usalama hata wakati usalama wa waathiriwa pia unapewa kipaumbele.
Kulikuwa na mkasa mwingine wakati maafisa wa Kenya Red Cross waliokuwa wakielekea Njabini kutoka Nakuru kusaidia katika uokoaji walipohusika kwenye ajali gari lao lilipogongana na lori karibu na soko la Kariamu, kwenye barabara kuu ya Ol Kalou kuelekea Njabini.
Mkuu wa matibabu katika Hospitali ya JM Memorial ambako maafisa hao 11 walipelekwa, Bw Samuel Mwaura, alisema mmoja alipata majeraha ya uti wa mgongo na anahitaji matibabu maalumu, mwingine alivunjika mguu na wa tatu akapata majeraha mabaya kichwani.
Bw Mwaura alisema wengine wanane walipata majeraha madogo na walikuwa wakiendelea kupokea matibabu.