• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
VITA DHIDI YA UFISADI: Uhuru apigwa breki

VITA DHIDI YA UFISADI: Uhuru apigwa breki

MAUREEN KAKAH na BENSON MATHEKA

MAHAKAMA ya kutatua mizozo ya wafanyakazi, imepiga breki agizo la Rais Uhuru Kenyatta la kuwataka wakuu wa idara za fedha na ununuzi katika wizara, idara na mashirika yote ya serikali kuondoka ofisini mara moja ili wakaguliwe upya.

Jaji Onesmus Makau alitoa uamuzi wa kusimamisha kwa muda agizo la Rais Kenyatta, kufuatia ombi la mwanaharakati Okiya Omtatah katika kesi ambayo amemshtaki Mkuu wa Utumishi wa Umma Bw Joseph Kinyua, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) na Mwanasheria Mkuu kwa kuwaagiza maafisa hao kuondoka ofisini.

Uamuzi huo wa korti unazima tangazo alilotoa Rais Ijumaa iliyopita wakati wa maadhimisho ya Madaraka Dei ambapo alisema maafisa wote wa ununuzi katika wizara na idara za serikali watafanyiwa ukaguzi ili kuondoa wanaoendeleza ufisadi.

Rais alitoa agizo hilo katika juhudi zake za kupiga vita ufisadi. Alisema kwenye ukaguzi huo, vifaa vya kutambua iwapo maafisa hao wanadanganya vitatumiwa.

Tangazo hilo lilifuatwa na barua ya Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua aliyewataka maafisa hao kuondoka mara moja, wawasilishe stakabadhi za mali, elimu na habari muhimu kwa serikali kufikia Ijumaa hii. Lakini jana Jaji Makau alisimamisha utekelezaji wa ilani hiyo ya Bw Kinyua.

“Kesi hii ikisubiri kusikilizwa na kuamuliwa, mahakama inatoa agizo la muda la kusimamisha ilani nambari No. OP/CAB.39/1A iliyotolewa na Bw Kinyua hadi Juni 13 kesi itakaposikilizwa kati ya pande zote,” alisema Jaji Makau.

Kulingana na Bw Omtatah, ilani ya Bw Kinyua ni kinyume cha sheria, ilitolewa haraka na bila kushirikisha umma kutoa maoni.

Alimlaumu Bw Kinyua akidai amekosa kazi ya kufanya na hatua yake ililenga kuonyesha kwamba vita dhidi ya ufisadi vinaendelea.

Alidai kwamba ilani ya Bw Kinyua ilizua taharuki katika utumishi wa umma huku maafisa hao wakihofia kupoteza kazi.

zao. “Ukaguzi hauhitaji mtu kuondoka ofisini isipokuwa awe anahujumiwa,” alisema Bw Omtatah.

Kwenye kesi yake, anasema mtu anafaa kuondoka ofisini baada ya kupigwa msasa na kupatikana hafai kushikilia ofisi fulani ya umma.

“Wakenya waliweka mfumo wa kisheria unaofaa kufuatwa na sio udikteta,” anasema Bw Omtatah kwenye kesi yake.

Mwanaharakati huyo anataka ilani hiyo ibatilishwe kabisa na kutangazwa kuwa haramu.

You can share this post!

Raila kusafiri Afrika Kusini kupatanisha Machar na Kiir

Familia za abiria wa ndege iliyotoweka zasubiri habari

adminleo