Kenya, Uganda na TZ zashuka viwango vya FIFA
Na GEOFFREY ANENE
HARAMBEE Stars ya Kenya imeteremka chini nafasi moja hadi nambari 112 kwenye viwango bora vya Shirikisho ka Soka Duniani (FIFA), ambavyo vimetangazwa Alhamisi.
Uganda imetupwa chini nafasi nane hadi nambari 82 duniani, Sudan imeshuka nafasi mbili hadi nambari 128 nayo Rwanda imeporomoka nafasi 13 hadi nambari 136.
Tanzania iko chini nafasi tatu hadi nambari 140, Burundi imeteremka nafasi mbili hadi nambari 148 nayo Ethiopia iko chini nafasi tano hadi nambari 151.
Malimbukeni Sudan Kusini, Djibouti, Eritrea na Somalia wamepaa nafasi moja kila mmoja hadi nambari 156, 197, 206 na 206, mtawalia.
Stars ya kocha Sebastien Migne, ambayo iko nchini India kwa Soka ya Hero Continental, iliteremka kutoka nafasi ya 111 hadi 112 baada ya kulemwa na Swaziland 1-0 Mei 25 na kunyamazisha Equatorial Guinea 1-0 Mei 28 mjini Machakos.
Ushindi wa Swaziland, hata hivyo, haukuwasaidia kuimarisha msimamo wao kwani wameshuka nafasi tatu hadi nambari 134 duniani. Equatorial Guinea imepaa nafasi mbili hadi nambari 143.
Wapinzani wa Kenya katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019, Ghana, Sierra Leone na Ethiopia wamepaa nafasi tatu hadi nambari 47, kuteremka nafasi nane hadi nambari 111 na kushuka nafasi tano hadi nambari 151, mtawalia.
Kuna mabadiliko mawili katika mduara wa 10-bora duniani ambapo Poland imeruka juu nafasi mbili hadi nambari nane nao mabingwa wa dunia mwaka 2010 Uhispania wameshuka nafasi mbili hadi nambari 10.
Ujerumani, Brazil, Ubelgiji, Ireno, Argentina, Uswizi na Ufaransa wamesalia katika nafasi saba za kwanza, mtawalia.
Tunisia inasalia nambari moja barani Afrika, lakini imetupwa chini nafasi saba hadi nambari 21 duniani.
Senegal ni nambari mbili Afrika. Imepaa nafasi moja hadi nambari 27 duniani.
DR Congo inasalia ya tatu Afrika na 38 duniani. Morocco inashikilia nafasi ya 41 duniani baada ya kuruka juu nafasi moja nayo Misri pia imepaa nafasi moja hadi nambari 45 duniani.
Katika mataifa yanayoshiri Hero Continental Cup, wenyeji India wamesalia katika nafasi ya 97 duniani. Ilizaba Chinese Taipei 5-0 Juni 1 na Kenya 3-0 Juni 4. Itapambana na New Zealand hapo Juni 7. New Zealand imeruka juu nafasi 13 hadi nambari 120 duniani nayo Taipei imeshuka nafasi mbili hadi nambari 123. Kenya na Taipei zitavaana uwanjani Mumbai hapo Juni 8. Timu mbili kutoka orodha ya India, Kenya, New Zealand na Taipei zitakabiliana katika fainali mnamo Juni 10.