Habari

ANGA YA KILIO: Mabaki ya ndege na miili ya watu 10 yapatikana msituni

June 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

HUZUNI na majonzi zilitanda Alhamisi ilipobainika kuwa abiria wote wanane na wahudumu wawili wa ndege iliyoanguka Msitu wa Aberdares mnamo Jumanne waliangamia wote katika ajali hiyo.

Kufikia Alhamisi jioni, maiti zote 10 zilikuwa zimepatikana kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo iliyoanguka ndani ya msitu huo eneo la Njabini, Kaunti ya Nyandarua.

Wahudumu wa ndege walioangamia ni marubani Kapteni Barbara Wangeci Kamau na msaidizi wake Jean Mureithi.

Abiria nao ni Ahmed Ali Abdi, Karaba Sailah Waweru Muiga, Khetia Kishani, Matakasakaraia Thamani, Matakatekei Paula, Ngugi George Kinyua, Pinuertorn Ronald na Wafula Robinson.

Afisa aelekeza jinsi ya kupanga miili ya watu 10 walioangamia kwenye ajali ya ndege katika eneo la Njabini Juni 7, 2018. Picha/ Evans Habil

Maiti zao zilizokuwa zimeharibika vibaya na zilisafirishwa hadi Nairobi ambapo utaratibu wa kuwatambua waliofariki unafanyika katika chumba cha maiti cha Lee.

Kifaa kinachonasa mawasiliano ya ndege (blackbox) pia kilipatikana.

Awali katika hoteli ya Weston jijini Nairobi, jamaa, familia na marafiki walikuwa na matumaini kuwa labda waathiriwa walikuwa wangali hai. Lakini matumaini yao yalikatizwa na tangazo la kampuni inayomiliki ndege hiyo ya Fly Sax.

“Tunasikitishwa na habari tunazopokea kutoka kwa makundi yaliyo eneo la ajali kwamba hakuna manusura,” mwenyekiti wa kampuni hiyo, Bw Charles Wako alisema.

Wakazi watazama kwa mshtuko na majonzi wasijue la kufanya baada ya watu wote kumi kuthibitishwa kuangamia kwa ajali ya ndege eneo la Njabini, kaunti ya Nyandarua. Picha/ Evans Habil

Jamaa wa waathiriwa walijawa na majonzi na vilio vikatanda kila mmoja akijiuliza maswali mengi.

“Yesu, nitapata wapi mume mwingine? Nani atawatunza watoto wangu? Mungu wangu mbona umeniwacha, ninakutumainia wewe!” Bi Margaret Wanjiru Kinyua alilia.

Alisema mumewe Kinyua alikuwa mfanyabiashara na alikuwa amesafiri Eldoret siku hiyo na baadaye kuelekea Kitale kwa biashara.

“Alinipigia simu mwendo wa saa tisa na dakika 39 jioni na tuliongea kwa muda. Alisema alikuwa karibu kuabiri ndege kurejea Nairobi. Kisha aliniuliza kuhusu watoto,” alieleza.

Aliongeza kuwa yeye pia alimuuliza kuhusu hali ya anga, na alimueleza kuwa ndege imechelewa kwa sababu ya hali mbaya ya hewa na lakini akampa moyo kuwa wangekuwa sawa.

Maafisa wasaidiana kuweka miili kwenye mifuko maalum tayari kwa usafirishaji hadi Kinangop ambapo ilipelekwa jijini Nairobi Juni 7, 2018. Picha/ Evans Habil

“Tuliongea hadi wakati alipokuwa akipanda ndege. Alistahili kuwa amefika saa kumi na moja jioni lakini simu yake ilikuwa imezima. Niliendelea kumpigia simu lakini ilikuwa bado haiingii,” alieleza. Marehemu Kinyua amewaacha watoto watatu wa miaka tisa, minne na miezi tisa.

Nayo familia ya Robinson Wafula ilieleza kuwa aliondoka Bungoma kwenda Nairobi kwa biashara. Dadake, Bi Charity Wafula alisema kakake, ambaye ni kifungua mimba, amemwacha mtoto mvulana wa miaka mitano.

Bw Kishan Khetia, 29, wa familia inayomiliki maduka makubwa ya Khetia Magharibi mwa Kenya pia alikuwa akielekea Nairobi kwa biashara za kawaida za familia alipokumbana na kifo chake.

“Alikuwa mwenye furaha alipoondoka nyumbani kuelekea kuabiri ndege na tulimtarajia kurejea nyumbani karibuni kuendelea na shughuli za kawaida. Ni vigumu kuamini kuwa ni miongoni mwa waliokufa kwenye ajali hii,” mjombake, Bw Ashok Khatia alieleza kwa simu.

Wakazi wabeba baadhi ya miili ya watu walioangamia kwenye ajali ya ndege kwenye milima ya Aberdares. Miili hiyo ilisafirishwa hadi mochari ya Lee jijini Nairobi Juni 7, 2018. Picha/ Evans Habil

Familia hiyo ilisafiri Nairobi baada ya kupata habari za kutoweka kwa ndege hiyo.

Familia ya Khetia ina maduka Eldoret, Kitale, Bungoma, Mumias na Kisumu miongoni mwa miji mingine ya Magharibi mwa Kenya.

Ndege hiyo aina ya Cessna C208 yenye nambari ya usajili 5Y-CAC, iliondoka uwanja mdogo wa Kitale katika Kaunti ya Trans Nzoia, Jumanne mwendo wa saa kumi na dakika tano jioni kuelekea Nairobi, lakini ilipoteza mawasiliano na waelekezaji wa safari za ndege mwendo wa saa kumi na moja na dakika 20 jioni.

Naibu Kamishna wa Kinangop, Bw Daniel Nyameti alisema kundi lililokuwa likitafuta ndege hiyo lilivunjika moyo sana kupata hakukuwa na manusura licha ya juhudi zao tangu Jumanne.

Ndege hiyo ilionekana jana saa kumi na mbili na dakika 45 alfajiri baada ya kutafutwa kupitia angani.

Hali ya anga eneo hilo pia iliripotiwa kuwa mbaya na kuathiriwa zaidi na ukungu, hali iliyotatiza utafutaji wake.

Ripoti ya Kennedy Kimanthi, Waikwa Maina, Stella Cherono na Barnabas Bii