Kipa apigwa marufuku kwa kudaganya ana jeraha ili kocha afurushwe
Na GEOFFREY ANENE
KIPA nambari moja wa Rayon Sport, Eric ‘Bakame’ Ndayishimiye amepigwa marufuku kwa muda usiojulikana kwa kupanga njama kocha Ivan Minnaert atimuliwe.
Kwa mujibu wa gazeti la Rwanda la New Times, Bakame alidanganya ana jeraha.
Taarifa nchini Rwanda zinasema kwamba viongozi wa klabu hii waliamua kupiga marufuku baada ya kugundua Ndayishimiye alijifanya ana jeraha ili asichezeshwe katika mechi ya ligi dhidi ya Musanze FC hapo Juni 8. Mechi hii ilimalizika 0-0 uwanjani Ubworoherane.
Gazeti hilo limeripoti kwamba Mrwanda huyu mwenye umri wa miaka 30 ameomba mashabiki na timu yake msamaha.
Mbali na kupigwa marufuku, Ndayishimiye pia amepokonywa unahodha, ambao umepewa raia wa Burundi, Pierrot Kwizera aliyekuwa naibu wa nahodha.
Katika mechi yake ya mwisho kama nahodha, gazeti hilo limesema, Rayon ililimwa 2-1 na wanyonge Amagaju uwanjani Amahoro. Inasemekana kipa huyu alihusika katika kipigo hicho, ambacho kilizima matumaini ya mabingwa hao kuhifadhi taji na kukasirisha mashabiki sana.
Majuzi, vyombo vya habari nchini Rwanda zilisema kwamba Mbelgiji Minnaert, ambaye aliwahi kunoa miamba wa Kenya, AFC Leopards, amepewa mwezi mmoja kuhakikisha Rayon inaandikisha matokeo mazuri la sivyo apigwe teke.
Rayon iko kundi moja na miamba wengine wa Kenya, Gor Mahia, katika Kombe la Mashirikisho la Afrika. Ilikabwa 1-1 na Gor nchini Rwanda mnamo Mei 6. Zitarudiana na Gor nchini Kenya mnamo Agosti 19.