HabariKimataifaSiasa

Mkutano wa Kim na Trump wapongezwa kote duniani

June 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

VIONGOZI wa mataifa mbalimbali duniani wamemiminia sifa mkutano wa kihistoria baina ya Rais wa Amerika Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un uliofanyika Jumanne nchini Singapore.

Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in alitaja mkutano huo kuwa wa kihistoria na uliofungua ukurasa mpya’

“Kim na Trump watakumbukwa kama marais walioandikisha historia kwa kudumisha amani ulimwenguni. Tumeacha siku za giza zilizogubikwa na vitisho vya kivita na sasa tumechukua mwelekeo mpya katika udumishaji wa amani,” akasema Moon.

Naye Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema: “Nimefurahishwa mno na maafikiano baina ya Rais Trump na mwenzake wa Korea kaskazini Kim kwa kukubaliana kukomesha utengenezaji wa makombora ya nyuklia.”

Serikali ya Denmark ilipongeza mkutano baina ya viongozi hao wawili lakini ikawataka Trump na Kim kuhakikisha kuwa mkataba wa kukomesha nyuklia uliotiwa saini unatekelezwa kikamilifu.

“Korea Kaskazini imewahi kukubali kusitisha utengenezaji wa makombora ya nyuklia lakini baadaye ikapuuza. Kuna haja ya kuhakikisha kuwa mkataba uliotiwa saini Jumanne unatekelezwa,” akasema Waziri Mkuu wa Denmark Løkke Rasmussen.

Rais wa China, Xi Ji Ping pia alipongeza mkutano huo wa kihistoria baina ya Trump na Kim.

Katika mkutano wa jana, viongozi hao wawili walisalimiana, wakafanya vikao vya faragha na kisha kutia saini mkataba wa maelewano.

Miongoni mwa masuala yaliyoafikiwa katika mazungumzo hayo ni kusitishwa kwa utengenezaji wa makombora ya nyuklia yaliyokuwa yakirushwa mara kwa mara na Korea Kaskazini.

Akihutubia wanahabari baada ya mkutano huo, Rais Trump alisema kuwa mataifa hayo mawili yataendelea na mazungumzo zaidi ili kuhakikisha kuwa mkataba huo unatekelezwa kikamilifu.

Rais Trump na Kim waliafikiana kuachana na vita vya maneno baina yao na badala yake wakaahidi kushirikiana kiuchumi.

Kim Jong-un amekuwa akishutumiwa kwa kuendeleza ugandamizaji wa haki za kibinadamu na mwaka jana alidaiwa kuagiza kuuawa kwa ndugu yake katika uwanja wa ndege nchini Malaysia.

Kim alikubali mwaliko wa Rais Trump wa kumtaka kuzuru ikulu ya White House nchini Amerika.

Ujumbe wa Trump ulijumuisha waziri wa Masuala ya Kigeni, Mike Pompeo, mshauri wa masuala ya usalama John Bolton na mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu ya White House John Kelly. Upande wa kiongozi wa Korea Kaskazini ulijumuisha mwandani wa Kim, Kim Yong Chol, ambaye alikutana hivi majuzi na Rais Trump katika White House.