• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Wanajeshi wa Uganda wazuilia polisi wa Kenya ziwani Victoria

Wanajeshi wa Uganda wazuilia polisi wa Kenya ziwani Victoria

Na RUSHDIE OUDIA

WANAJESHI wa Uganda wanawazuilia maafisa wa usalama wa Kenya katika kile kinachoonekana kuwa mzozo wa hivi punde kuhusu mvutano wa uvuvi kwenye Ziwa Victoria.

Maafisa hao walikamatwa Jumatatu na silaha zao kutwaliwa na wanajeshi wa UPDF karibu na visiwa vya Mageta na Hama kwenye ziwa hilo. Kisha wakapelekwa hadi taifa hilo jirani kwa boti.

Mashahidi waliambia Taifa Leo kwamba bunduki za maafisa hao zilitwaliwa sawa na simu zao kabla yao kufululizwa hadi gereza la Bugiri Mainland mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Mkuu wa Polisi wa Utawala katika Kaunti ya Siaya, Bw Patrick Lumumba alisema kisa hicho kilichotokea saa tisa alasiri kilihusisha takriban wanajeshi wanane waliokuwa wakishika doria.

Maafisa hao wa Kenya, alieleza Bw Lumumba, walizingirwa na kukusanywa pamoja na wavuvi wa Kenya walionaswa wakivua samaki katika maji ya Uganda.

Alisema wavamizi hao waliokuwa wamejihami kwa silaha kwanza walitekwa nyara boti tano za Kenya na kutoa injini zao.

“Maafisa wetu walizidiwa nguvu na wavamizi hao waliowadhania kuwa ni raia na wavuvi,” alieleza.

Kamishna wa Kanda ya Nyanza, Bw Moffat Kangi, alitarajiwa kuzuru eneo hilo kujaribu kuleta upatanisho.

Ni kisa cha pili cha aina yake ambacho kimetekelezwa na maafisa wa Uganda wanaoshika doria kwenye ziwa hilo.

Novemba mwaka jana, wizara ya kigeni ililazimika kuingilia kati baada ya wavuvi 17 wa Homa Bay kukamatwa na kisha kuzuiliwa nchini Uganda kwa madai ya kuvua samaki bila idhini.

Baadhi ya waliozuiliwa walidai kuwa walilazimishwa kulipa faini kabla kuachiliwa.

Ingawa Kenya hutuma kikosi cha maafisa wa polisi kushika doria katika Ziwa Victoria, Uganda imetumia wanajeshi wa kitengo maalum cha Special Forces Command ambacho ni sehemu ya jeshi la Uganda (UPDF).

Mwezi Februari, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema yeye huwatuma wanajeshi kushika doria ziwani humo kwa sababu maafisa wake wa polisi na majini ni wafisadi mno kiasi kwamba hawaaminiki kulinda samaki wa Uganda.

Wakati huo huo katika Kaunti ya Siaya, wavuvi walisusia kazi na kusema hawatafanya tena mikutano yoyote mingine.

Badala yake wanataka serikali itume kundi la maafisa wa usalama wa kushika doria wenye silaha za kisasa zinazowiana au kuzidi zile za maafisa wa Uganda.

Mbunge wa Bondo Gideon Ochanda alishutumu kujikokota kwa serikali ya Kenya kuchukua hatua zozote kuhusiana na suala hilo.

“Inasikitisha sana kwamba maafisa wa usalama wa Kenya wanazuiliwa kinyume cha sheria katika taifa jirani ilhali serikali haijatoa taarifa yoyote,” akasema Bw Ochanda.

You can share this post!

Wabunge wa Zambia wazuru Kenya kufunzwa mbinu za kuzima...

Ruto akerwa na bei ghali ya mashamba jijini Nairobi

adminleo