RAMADHANI: Biashara yanoga Mwezi Mtukufu ukifika ukingoni
NA KALUME KAZUNGU
WANABIASHARA katika kisiwa cha Lamu wanavuna pakubwa msimu huu ambapo Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unatarajiwa kutamatika mwishoni mwa juma hili.
Awali, wanabiashara walilalamikia uchache wa wateja wao punde Ramadhani ilipoanza mnamo Mei mwaka huu.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo juma hili aidha ulibaini kuwa idadi ya wateja wanaojitokeza kununua mapochopocho tayari kwa matayarisho ya Idd-Ul-Fitr ilikuwa imeongezeka maradufu kufikia Jumatano.
Wanabiashara ambao wamekiri kuvuna pakubwa ni wale wa maduka ya nguo, mapambo, mboga, waendeshaji boti na makampuni ya mabasi ya usafiri wa umma wanaohudumu kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Mombasa.
Baadhi ya wanabiashara waliohojiwa walisema wateja wamekuwa wakimiminika kwenye vibanda vya nguo na mboga kununua bidhaa kwa matayarisho ya sherehe ya Iddi inayotarajiwa kuadhimishwa mwishoni mwa juma hili.
“Tunashukuru. Punde Ramadhani ilipoanza wateja walipotea kabisa. Wakati huu ambapo tunatarajia Radhamani kufikia ukingoni, tumeshuhudia wateja wengi wakimiminika kwenye maduka na vibanda vyetu kujinunulia bidhaa tayari kwa sherehe za Iddi,” akasema Bi Fatma Mohamed ambaye ni mfanyibiashara wa duka maarufu la nguo katika mtaa wa Langoni mjini Lamu.
Wahudumu wa mabasi ya usafiri wa umma pia walikiri kupata abiria wengi msimu huu ambapo Ramadhani inaelekea ukingoni.
Bw Said Swale anasema abiria wengi wamekuwa wakiingia na kutoka Lamu hasa tangu juma hili lilipoanza.
“Tumekuwa tukipata abiria wengi juma hili. Kuna wanafamilia ambao wamesafiri kuja Lamu kutoka Mombasa, Malindi na Mambrui ili kujumuika na ndugu, jamaa na marafiki katika kusherehekea Iddi-Ul-Fitr. Pia kuna wale wanaotoka hapa Lamu kuelekea miji mingine ya Pwani na hata Nairobi ili kuadhimisha hafla ya Iddi. Biashara iko sawa,” akasema Bw Swale.
Wakati huo huo, msongamano mkubwa wa wakazi na punda unazidi kushuhudiwa hasa nyakati za jioni kwenye mji wa kale wa Lamu hasa tangu juma hili lilipoanza.
Waendeshaji mikokoteni wanaohudumu kwenye vichochoro vya mji wa Lamu wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu hasa kila jioni ambapo barabara na vichochoro huwa vimefungana kutokana na idadi kubwa ya punda na wakazi wanaotumia barabara hizo.
Bw Mohamed Maulana ambaye ni mwendeshaji rukwama alisema msongamano unaoshuhudiwa umeathiri pakubwa shughuli zao huku wakilazimika kutumia muda mwingi vichochoroni.
“Tangu Ramadhan ilipoanza, wakazi wengi hujitokeza zaidi jioni wakitafuta mlo ili kufuturu. Wanabiashara pia wamekuwa wengi vichochoroni na kupelekea msongamano zaidi. Serikali ifikirie jambo hili kwani limeanza kusababisha athari kwa watumiaji wa barabara hasa sisi waendeshaji mikokoteni,” akasema Bw Maulana.