• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
URUSI 2018: Ujerumani kukaa ange kutetea ubingwa

URUSI 2018: Ujerumani kukaa ange kutetea ubingwa

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA watetezi wa Kombe la Dunia, Ujerumani ni miongoni mwa mataifa yatakayoelekezewa jicho la karibu sana nchini Urusi baada ya kusuasua kwao katika mechi nyingi za hivi karibuni kuzua maswali mengi kuhusu utayarifu wao katika jitihada za kulihifadhi taji la mwaka huu.

Chini ya kocha Jaochim Loew, Ujerumani wametiwa kwenye zizi moja na Mexico, Uswidi na Korea Kusini wanaokamilisha Kundi F.

Iwapo Ujerumani watasonga mbele kutoka hatua ya makundi, basi watakutana ama na Uswizi, Serbia, Costa Rica au Brazil wanaotarajiwa kukitawala kilele cha Kundi E.

Ujerumani ambao ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia wanaamini kuwa watamaliza kundi lao katika nafasi ya kwanza ama, hali ikiwa mbaya sana kwao, basi waambulie nambari mbili.

Nafasi hizi mbili za kwanza katika mechi za makundi zitawapa Ujerumani tiketi ya kutinga raundi ya 16-bora.

Rekodi nzuri inayojivuniwa na Ujerumani dhidi ya wapinzani wake wote katika Kundi F inampa Loew afueni tele japo uthabiti wa kikosi chake kinazidi kutiliwa shaka baada ya kupoteza msururu wa michuano ya kupimana nguvu.

Kabla ya kubamizwa 2-1 na Austria majuma mawili yaliyopita, kikosi hicho cha Loew kilipokezwa kichapo cha 1-0 na Brazil kwenye mchuano wa kirafiki uliowakutanisha jijini Brazil mnamo Machi 2018.

Afueni ya pekee kwa Ujerumani ni kupona kwa kipa wao nambari moja, Manuel Neuer ambaye Loew amedokeza uwezekano wa kutegemea pakubwa huduma zake nchini Urusi baada ya kupona jeraha lililomweka nje kwa miezi minane iliyopita.

Ujerumani wanatazamiwa kushuka dimbani kupepetana na Mexico jijini Moscow katika mechi ya ufunguzi wa Kundi F kwenye Kombe la Dunia mnamo Juni 17.

Timu nyingine ambayo maandalizi yake yametiliwa shaka ni Argentina ya kocha Jorge Sampaoli. Maandalizi ya Argentina kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu yamevurugwa na panda-shuka tele, tukio la hivi karibuni zaidi likiwa ni pigo la kujeruhiwa kwa nyota Manuel Lanzini wa West Ham United ambaye kwa pamoja na kipa Sergio Romero wa Man-United, sasa hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Sampaoli nchini Urusi.

Changamoto

Baada ya kufutiliwa mbali kwa mchuano wa kirafiki uliokuwa uwakutanishe Argentina na Israel mwishoni mwa wiki jana, vijana wa Sampaoli walielekea Urusi na kupiga kambi mjini Bronnitsy, kilomita chache kutoka jijini Moscow. Argentina wanapigiwa upatu wa kujinyanyua kwenye makala ya Kombe la Dunia mwaka huu hasa ikizingatiwa kwamba ni fursa ya mwisho kwa Messi kuvalia jezi ya timu ya taifa.

Kikosi hicho kilizidiwa maarifa na Ujerumani kwenye fainali ya 2014 iliyowakutanisha nchini Brazil.

Mwaka mmoja baadaye, Argentina walichabangwa na Chile kwenye fainali ya Copa America kabla ya wapinzani hao wao kuwapiga tena katika fainali ya Copa America mnamo 2016.

Kusuasua kwa Argentina katika safari ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu kulimweka kocha Edgardo Bauza katika ulazima wa kujiuzulu na pengo lake kujazwa na Sampaoli. Miamba hao wa soka ya Amerika Kusini wamepangwa pamoja na Iceland, Croatia na Nigeria kwenye Kundi D. Katika juhudi za kuijaza nafasi ya Lanzini, Sampaoli amemuita kambini nyota Enzo Perez River Plate ambaye kwa sasa atashirikiana na Angel Di Maria, Gonzalo Higuain na Sergio Aguero katika safu ya mbele.

You can share this post!

URUSI 2018: Mastaa watakaonogesha dimba

URUSI 2018: Fahamu vikosi vya timu zote zinazocheza fainali

adminleo