Mtaalamu aonya dhidi ya kuharakisha kupyesha mtaala
Na CECIL ODONGO
MKURUGENZI wa Kituo cha Hesabu, Teknologia na Sayansi ya Elimu barani Afrika(CEMASTA) Bw Stephen Njoroge amewashauri walimu wakuu katika shule za msingi na upili wasiharakishe kukamilisha mtaala wa elimu akisema hilo linawapa wanafunzi msingi hafifu wa kimasomo.
Alisisitiza kwamba wanafunzi wanaposomeshwa kulingana na kanuni zinazotakikana kufuatwa kwenye mtaala, wao hupata uelewaji mpana wa mada wanayosomeshwa kulingana na muda toshelezi uliowekwa na Taasisi ya Ukuzaji Mtaala nchini (KICD) na Wizara ya Elimu.
Akizungumza wakati wa mahojiano katika CEMASTA , Bw Njoroge alisema kwamba kuharakishwa kumalizwa kwa silabasi kunaponza uelewaji wa wanafunzi kuhusu mada muhimu yanayohitaji muda wa kutosha katika kila somo shuleni.
Taasisi ya CEMASTA inawapa malezi na mafunzo ya kitaalam walimu wa masomo ya hesabu na sayansi ili kufundisha vizuri masomo hayo wakizingatia kanuni na maagizo yaliyoko kwenye mtaala.
Kwa upande wake, Naibu mkurugenzi anayesimamia kitengo cha huduma za mtaala wa utafiti katika KICD Jacqueline Onyango aliunga mkono kauli ya Bw Njoroge akisema kutekelezwa kikamilifu kwa silabasi inahakikisha wanafunzi wanaelewa vizuri wanayofunzwa darasani.
Aliongeza kwamba walioimarisha mtaala walitoa muda wa mapumziko kwa wanafunzi katika ratiba inayodumu kati ya saa mbili hadi kumi jioni . Ratiba hiyo inasheheni vipindi vya mapumziko wakati wa chakula cha mchana na katikati mwa vipindi vya masomo.
Hata hivyo alisikitikia hatua za baadhi ya walimu wa shule nchini kuwalazimisha wanafunzi kushiriki masomo ya ziada wakilenga kukamilisha silabsi mapema kuliko muda uliowekwa na wizara ya elimu kwenye mtaala.
Aidha alisisitiza kwamba ujuzi na hekima zinazopatikana kutokana na masomo darasani zinafaa kuwasaidia wanafunzi hao baadaye kujiendeleza kimaisha.
“Wanafunzi wanahitajika kutumia ujuzi wanaopata shuleni hata baada ya kukamilisha masomo yao. Masomo hayahusishi tu kuuliza na kujibu maswali katika mitihani ya kitaifa,” akasema Bi Onyango.