Benki zilizofanikisha ufisadi NYS kuona cha moto
Na CHARLES WASONGA
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji amesema benki ambazo zilitumika kufanikisha wizi wa pesa za umma zitachunguzwa na kuadhibiwa.
Bw Haji aliwaambia maseneta Jumatano kwamba benki hizo ni zile ambazo zilitumika katika wizi wa Sh9 bilioni katika Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) na kashfa ya ununuzi wa ardhi ya shule katika eneo la Ruaraka ambapo Sh1.5 bilioni ziliporwa.
“Katika kesi ya NYS tulibaini kuwa zaidi ya Sh100 milioni zilitolewa katika benki mbalimbali kwa siku tatu huku katika sakata ya ardhi ya Ruaraka Sh250 milioni zikitolewa kwa muda wa siku tatu, huku sehemu za fedha hizo zikihamishwa hadi taifa la Mauritius ilhali hizi ni pesa za umma.
Baada ya fedha kutolewa huwa ni vigumu kuipata tena,” Bw Haji akaambia wanachama wa kamati ya Seneti kuhusu Sheria alipofika mbele yao katika majengo ya bunge.
“Tunashirikiana na Benki Kuu ya Kenya (CBK), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Tume ya Maadili na Kupambana Ufisadi (EACC) na Kitengo kupambana na ufisadi katika sekta ya benki (AFU) kuchunguza ikiwa kuna maafisa wa benki hizo walishirikiana na wezi hao kufanikisha wizi wa pesa za umma.
Tunaendesha uchunguzi huo na hivi karibuni tutawanasa,” DPP akaambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Nandi Bw Samson Cherargei.
Bw Haji alisema katika kesi ya wizi wa Sh9 bilioni katika NYS, benki 10 zinachunguzwa na katika sakata ya ardhi ta Ruaraka zaidi ya benki saba zinamulikwa ambapo zitaadhibiwa endapo zitapatikana na hatia ya kuendeleza ufisadi.
Mkurugenzi huyo pia alisema maafisa wake watashirikiana na wapelelezi wa EACC ili kuhakikisha kuwa ushahidi tosha unakusanywa kuhusu kesi za ufisadi.
“Hatutaki hali ambapo afisi yangu inalazimika kurudisha faili kwa EACC kwa misingi ya kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha kuhimili kesi mahakamani,” akasema Bw Haji.
Alisema washukiwa katika sakata ya NYS waliweza kufunguliwa mashtaka haraka kwa sababu afisi yake ilishirikiana na vitengo vingine katika uchunguzi wa kesi hizo.