• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Wanachuo wakamatwa wakipika keki zenye bangi kuuzia wenzao

Wanachuo wakamatwa wakipika keki zenye bangi kuuzia wenzao

Na GEORGE SAYAGIE

WANAFUNZI wawili wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara walikamatwa na polisi mjini Narok baada ya kupatikana wakipika keki walizoweka bangi ili kuwauzia wanafunzi wenzao.

Wanafunzi hao walio na umri wa miaka 23 na 25, walikamatwa wakiwa katika chumba chao mita chache kutoka lango kuu la chuo hicho mnamo Jumamosi wakiendelea kuandaa keki hizo.

Iliripotiwa washukiwa hao walikuwa wakichunguzwa na polisi kwa muda

Mkuu wa upelelezi Kaunti ya Narok (CCIO) Bw Zachary Kariuki, ambaye aliongoza msako wa kuwakamata washukiwa hao, alisema walipata vipande 56 vikiwa tayari.

“Tulipata habari kutoka kwa umma na walinzi wa chuo kikuu kwamba kulikuwa na biashara haramu katika chumba kimoja. Tumekuwa tukichunguza kwa wiki moja na leo tulifaulu kuwakamata,” alisema Bw Kariuki.

Alisema kuwa matumizi ya dawa za kulevya yameongezeka karibu na chuo hicho.

“Keki hizi zinapotumiwa, mtu hulewa kwa zaidi ya saa 12 akiwa hajitambui. Huwa wanawaeleza wateja wao kwamba hawafai kutumia zaidi ya moja na kwamba hawafai kunywa pombe baada ya kula keki hizi,” alisema.

Afisa huyo aliwaonya wenye nyumba za kukodisha kwamba hawafai kuruhusu zitumiwe kwa biashara haramu akisema wanaweza kukamatwa na kushtakiwa. Alisema washukiwa watafikishwa kortini leo kufunguliwa mashtaka.

Afisa anayesimamia ulinzi katika chuo hicho Bw David Muiruri alisema kukamatwa kwa wanafunzi hao wawili ni hatua kubwa katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya chuoni. Alikiri kwamba matumizi ya mihadarati yamekuwa yakiongezeka chuoni.

“Tunawaomba wanafunzi kuripoti kwetu watu wanaoshuku kuwa wauzaji wa dawa za kulevya ili tuweze kupigana na biashara hii haramu,” alisema.

You can share this post!

Al Shabaab waua polisi 8 kwa bomu Wajir

Seneta Mkenya ajipata kwa kashfa ya pesa Australia

adminleo