Daktari mwizi sugu wa mioyo ya wafu motoni
Na ISABEL GITHAE
MPASUAJI mkuu wa zamani wa maiti serikalini (pichani) Moses Njue Jumatatu alifikishwa katika Mahakama ya Meru kushtakiwa kwa tuhuma za kuiba moyo wa mtu aliyefariki.
Mahakama iliambiwa kuwa mnamo Machi 12, 2015, katika Hospitali ya Consolata iliyoko Meru, aliiba moyo wa Benedict Karau alipokuwa akifanyia mwili wake upasuaji wa kubainisha chanzo cha kifo.
Hii si mara ya kwanza kwa mpasuaji huyu kushtakiwa kwa kuchukua moyo wa maiti kwa njia zinazokiuka sheria.
Mnamo Mei, Dkt Njue alikanusha madai mengine kama hayo aliposhtakiwa kwa kuiba moyo wa marehemu Timothy Mwandi Muumbo katika hifadhi ya maiti ya Lee, Nairobi Juni 25, 2015. Alikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 pesa taslimu.
Jana alipofikishwa mbele ya Jaji Lucy Ambasi, alikanusha mashtaka matatu aliyosomewa.
Shtaka la pili lilihusu kuharibu moyo wa marehemu. Upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba katika siku tofauti kuanzia Machi 12 hadi Septemba 18, 2015 katika hifadhi ya maiti ya Meru, Dkt Njue aliharibu moyo huo baada ya kuuiba kwani alifahamu kuwa ungehitajika kutumiwa kama ushahidi.
Shtaka la tatu alilokanusha lilikuwa kuhusu kuondoa moyo huo mwilini mwa marehemu kwa njia haramu.
Wakili wake, Bw Victor Andande, aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana.
Mahakama iliagiza aachiliwe kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu au bondi ya Sh2 milioni na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.
Kesi hiyo imepangiwa kutajwa mnamo Juni 28 na kusikilizwa mwezi Agosti tarehe 6, mwaka huu.