FKE yapinga wafanyakazi kutozwa ada ya kujenga nyumba
Na BERNARDINE MUTANU
Shirikisho la Waajiri nchini(FKE) limepinga pendekezo la Hazina ya Fedha la kutoza wafanyikazi asilimia 0.5 ya mshahara wao kufadhili maendeleo ya nyumba.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa FKE Jacqueline Mugo alisema pendekezo hilo halistahili.
Katika pendekezo hilo, Waziri wa Fedha Henry Rotich alisema kuwa hazina hiyo itasaidia wananchi kumiliki nyumba kote nchini.
Mkurugenzi huyo alisema waajiri hawakutarajia pendekezo hilo ambalo linatarajiwa kuwafinyilia zaidi wafanyikazi na waajiri.
“Itakuwa vigumu sana kwetu kuunga mkono pendekezo hilo kwa sababu hatujui utaratibu uliofuatwa ili kufikia kiwango hicho,” alisema Jumatano.
Alisema kuwa hakuna hakikisho kwamba wafanyikazi na waajiri watafaidishwa na pendekezo hilo.
Wakenya walioajiriwa rasmi wamekuwa wakichangia hazina ya Hospitali (NHIF) na ile ya malipo ya uzeeni, na hiyo itakuwa hazina ya tatu kwao kuchangia.