• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Vyuo vyatakiwa kubuni ofisi za kusaidia wanafunzi kuhusu ajira

Vyuo vyatakiwa kubuni ofisi za kusaidia wanafunzi kuhusu ajira

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu Amina Mohamed ameamuru vyuo vikuu na vyuo vya kadri kote nchini kuanzisha afisi za kuwashauri wanafunzi kuhusu mahitaji ya soko la ajira (Offices of Career Services-OCS) kuanzia mwezi Julai.

Alisema huduma zitakazotolewa katika afisi hizo zitawawezesha wanafunzi kupata ajira kwa urahisi baadhi ya kukamilisha kozi zao, hatua ambayo itapunguza tatizo la sasa ambapo idadi kubwa ya vijana hawana ajira baadhi ya kuhitimu kwa shahada za juu.

“Takriban vijana milioni moja hutimu kila mwaka kutoka vyuo vikuu na vyuo vingine vya kadri. Lakini inasikitisha kuwa ni mmoja pekee kati ya watano kuweza kupata ajira katika sekta ya umma. Idadi kubwa hukosa ajira kwa sababu ya kukosa ujuzi na maarifa zinazohitajika katika soko la ajira nyakati hizi,” akasema Bi Mohamed.

Akaongeza: “Hii ndio maana Wizara yangu kwa ushirikiano na vyuo husika na wahisani wengi imebuni mpango huu wa kuanzishwa kwa afisa maalum za kutoa mwongozo na ushauri kwa wanafunzi kuhusu kozi ambazo zitawapa ujuzi na maarifa zinazolandana na mahitaji ya soko la ajira.”

Bi Mohamed alivitaka vyuo hivyo kutumia sehemu ya bajeti zao kufadhili uanzishwaji wa afisi hizo katika mabewa yao huku akiongeza kuwa wizara yake itavipa rasilimali zinazohitajika, “endapo patatokea haja ya kufanya hivyo.”

Waziri huyo alisema hayo Alhamisi alipozindua mpango huo kuanzishwa kwa afisi hizo, katika hafla iliyoandaliwa katika ukumbi wa Taifa Hall, katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Bi Amina ambaye aliandamana na Waziri Msaidizi Simon Kachapin na makatibu katika wizara hiyo, alisema mpango huo ni sehemu ya mabadiliko ambayo serikali imeanzisha katika sekta ya elimu ya juu.

“Wanafunzi wataelekezwa na kufundishwa mbinu ambazo zitawawezesha kupata ajira kwa urahisi. Hii ina maana mitaala ya masomo katika vyuo vya masomo ya juu vitahitaji kufanyiwa mabadiliko ili kulandana na mahitaji ya ulimwengu wa sasa pamoja na malengo ya maendeleo nchini Kenya,” akasema.

You can share this post!

SHANGAZI: Nimegawia wengi asali lakini sijawahi kuhisi utamu

KDF wanatuhangaisha usiku,walia wakazi wa Mpeketoni

adminleo