IGAD yabuni sera kurahisishia wanachama wake biashara mipakani
Na BERNARDINE MUTANU
JUMUIYA ya Mamlaka ya Kimataifa kuhusu Maendeleo (IGAD) imepitisha sera ya biashara isiyo rasmi nje ya mipaka pamoja na usimamizi wa pamoja wa kiusalama miongoni mwa mataifa husika.
Sera hiyo ilipitishwa Ijumaa na mawaziri kutoka mataifa husika na itawasilishwa kwa marais wa IGAD kabla ya kuwasilishwa kwa Muungano wa Afrika (AU).
Mawaziri hao kutoka Kenya, Djibouti, Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, Somalia na Uganda walikutana Mombasa, Kenya walikopitisha sera hiyo.
Viongozi hao walisema sera hiyo itasaidia katika kuimarisha eneo la biashara huru Barani Afrika (FTA).
Mnamo Machi 21, zaidi ya mataifa 40 kutoka Afrika yalitia sahihi mkataba wa kuunda FTA ili kuimarisha biashara kati ya mataifa washirika.