Habari Mseto

Afueni serikali za kaunti kuongezewa muda kukagua madeni

June 25th, 2018 1 min read

 Na BERNARDINE MUTANU

Hazina ya Kitaifa ya Fedha imetoa idhini kwa magavana kumaliza kukagua madeni kufikia mwishoni mwa wiki.

Hatua hiyo ni kwa lengo la kuziwezesha serikali za kaunti kulipa madeni yake. Hatua hiyo ni afueni kwa maelfu ya wafanyibiashara, watoaji huduma na wanakandarasi ambao wanadai serikali za kaunti.

Kila serikali inatarajiwa kuunda kamati za kiufundi kukagua na kudhibitisha madeni katika mkataba ulioafikiwa kati yake na Hazina ya Fedha.

“Tumeagiza maafisa wote wa kuhasibu matumizi ya fedha kumaliza utaratibu huo kabla ya mwisho wa mwezi huu,” alisema Waziri wa Fedha Henry Rotich Ijumaa.

Alisema kaunti zinafaa kumaliza madeni yote kwanza kabla ya kuingia katika mikataba mipya na wafanyibiashara.

Ripoti ya Mratibu wa Bajeti ilionyesha kuwa gatuzi zilikuwa na madeni ya Sh100 bilioni kufikia mwisho wa mwaka wa kifedha wa 2014/15.