• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Wembe wa kumnyoa Jumwa sasa watiwa makali bungeni

Wembe wa kumnyoa Jumwa sasa watiwa makali bungeni

Na CHARLES WASONGA

AZMA ya chama cha ODM ya kutaka kumwondoa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa kutoka Tume ya Huduma za Bunge (PSC) imepigwa jeki baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kutoa mwongozo kuhusu namna ya kuifanikisha.

Akijibu barua ya kiranja wa wachache Junet Mohamed iliyomwomba kuishauri ODM kuhusu utaratibu wa kumwondoa kamishna wa PSC, Bw Muturi alisema hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kupitia hoja ambayo itahitaji kupitishwa na idadi kubwa wala sio thuluthi mbili ya idadi ya wabunge.

“Nimepokea ombi linalopendekeza kuondolewa kwa Bi Jumwa kutoka wadhifa wake kama kamishna wa PSC. Utaratibu wa kutelekeza hatua hiyo umeelezwa katika kipengee cha 127 cha Katiba. Hii ni kupitia hoja ambayo sharti iungwe mkono na wabunge wengi wa mujiubu wa kipengee cha 122 cha katiba,” Bw Muturi akasema kwenye barua aliyomwandikia Bw Mohamed.

Sasa kiranja huyo atahitajika kuandaa hoja maalum huku akielezea bayana sababu za kutaka kumwondoa Bi Jumwa kutoka PSC, sababu ya kwanza ikiwa ni hatua yake ya kuunga mkono azma Naibu Rais William Ruto kuwa Rais mwaka wa 2022.

Alhamisi, Bw Mohamed ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki, alisema ataandaa hoja hiyo “haraka iwezekanavyo kwani nidhamu sharti idumishwe ndani ya ODM.”

“Nafurahi kuwa Spika Muturi ametoa mwelekeo kuhusu suala hili lenye umuhimu kwetu kama chama. Bila kupoteza wakati nimeanza kuandaa hoja hiyo ambayo nitaiwasilisha bunge wakati wowote kuanzia juma lijalo ili wabunge walijadili.

Ni kinyume cha Katiba kwa mtu kuendeleza sera za vyama viwili vya kisiasa kwa wakati mmoja,” akasema Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa karibu wa kiongozi wa chama hicho, Raila Odinga.

Akaongeza: “Vile vile, tutaanza kuwaadhibu wabunge wengine ambao wamekaidi msimamo wa chama chetu wa kutojihusisha na kampeni za 2022 bali mpango wa kupalilia umoja nchini kama ilivyoanishwa kwenye muafaka kati ya kiongozi wetu Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, Bi Jumwa ameshikilia kuwa hatatishwa na yeyote na kwamba ataendelea kumuunga mkono Naibu Rais “hata kama ODM itadhamini mgombeaji wa urais 2022.”

“Sijatenda kosa lolote dhidi ya chama… hamna mgogoro wowote kati yangu na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Hatua yangu ya kutangamana na watu wengine ni sehemu ya mpango wa kuendeleza moyo wa salamu ulioanzishwa na Raila.”

alinukuliwa kusema juzi akiwa mjini Malindi.

Mnamo Jumatano, bunge kadhaa wa Pwani walikariri kuwa wataendelea kumuunga mkono Bw Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022. Walisema hawajapa habari zozote kuhusu mipango ya kujadiliwa kwa mienendo ya Bi Jumwa.

“Kwa sasa Bw William Ruto ni Naibu Rais nchini Kenya na tutaendelea kufanya kazi naye.” akasema Mbunge wa Bura Ali Wario kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

You can share this post!

JUBILEE YATOKOTA: Joto kali huku wandani wa Uhuru na Ruto...

MKASA WA GIKOMBA: Moto uliwashwa makusudi, wadai...

adminleo