• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Uswizi kurejeshea Kenya pesa za umma zilizofichwa na wezi

Uswizi kurejeshea Kenya pesa za umma zilizofichwa na wezi

Na LUCY KILALO

USWIZI imeahidi kurejesha mabilioni ya pesa zilizotokana na ufisadi ambazo zimefichwa nchini humo.

Hatua hiyo ilifuatia mazungumzo Jumatatu kati ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Uswizi, Alain Berset (pichani) ambaye yuko nchini kwa ziara rasmi ya siku mbili.

Marais hao wawili walitia saini Mkataba wa Maelewano kuhusu utaratibu utakaoongoza kurejesha mali iliyotokana na ufisadi na uhalifu nchini Kenya. Harakati hiyo pia inaungwa mkono na Uingereza na Kisiwa cha Jersey, na itasaidia Kenya kupata pesa zilizoibwa na wafisadi na kisha kufichwa katika nchi hizo tatu.

“Uswizi iutarudisha pesa ambazo zimezuiliwa hasa kutokana na kashfa kama ya Anglo Leasing. Uswizi na Kenya zinakubaliana kwa lengo moja katika vita dhidi ya ufisadi,” alisema rais Berset katika mkutano wa pamoja na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Uswizi ilikuwa imezuilia pesa zilizohusiana na kashfa hiyo huku kesi ikiendelea hapa nchini. Hata hivyo, hilo litaweza kufanyika baada ya kukamilika kwa kesi hiyo.

“Nina furaha kuwa baada ya mashauriano, tumeafikiana kuhusu utaratibu wa kurejesha pesa. Hatua ya kurudisha pesa hizo imeaanza,” alisema.

Rais Kenyatta alisisitiza kuwa ufisadi hautavumiliwa nchini, huku akisema kuwa unanyima nchi na vizazi vyake hali ya maisha inayostahili.

Alieleza kuwa kunaswa kwa mali inayotokana na ufisadi husaidia kudhibiti ufisadi, huku akieleza pia kuwa pesa hizo zitatumika kuboresha nchi.

Mapema mwaka huu, Uswizi ilielezea kunasa kwa mali yenye thamani ya Sh200 milioni iliyohusiana na kashfa ya Anglo Leasing. Nchi hiyo ilieleza kuwa iko tayari kurejesha mali hiyo muda tu mahakama ikitamatisha kesi.

Utaratibu huo ambao unalingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ufisadi, unatoa mwongozo wa kuchukua mali iliyoibwa. Katika ushirikiano huu, mali ya kwanza inayolengwa niiliyotokana na kashfa ya Anglo Leasing, ambayo kesi yake ingali inaendelea humu nchini.

Mwongozo huo unaelekeza kuwa hatua za kuchukua mali zilingane na maamuzi yanayotolewa na mahakama. Pia unaeleza kuwa mali inayopatikana itumike kwa miradi ya maendeleo ambayo tayari imetambuliwa, kama katika sekta ya afya, ambayo itawafaidi Wakenya.

Pia kamati itaundwa ambayo itajumuisha afisi ya rais, Hazina Kuu., Mwanasheria Mkuu, Kitengo cha Kusaka Mali, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi na mabalozi ama waakilishi wa nchi zinazohusika katika mkataba.

Mapema mwaka huu, Uswizi pia ilitia saini Mkataba wa Maelewano na Nigeria kutoa nafasi ya mali iliyopatikana kinyume cha sheria irejeshwe nchini humo.

Nchi hiyo mnamo Desemba 2017, ilisema kuwa itarejeshea Nigeria mali yenye thamani ya zaidi ya Sh32 bilioni iliyonaswa kutoka kwa familia ya aliyekua kiongozi wa kijeshi Sani Abacha.

You can share this post!

Serikali kukusanya taarifa za Wakenya wenye jinsia mbili

Wanaounga mkono Ruto Pwani waonywa

adminleo