Makala

KAULI YA MATUNDURA: Wahakiki wa Fasihi walivyombughudhi Wole Soyinka, kawaita machichidodo

July 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BITUGI MATUNDURA

WOLE Soyinka, Ali Mazrui , William Robert Ochieng’ na Ngugi wa Thiong’o ni wasomi ambao maoni yao yalivutia sana vyombo vya habari – hasa magazeti kila walipotoa kauli yoyote kuhusu fasihi, siasa, lugha na utamaduni.

Kwa bahati mbaya Maprofesa Mazrui na Ochieng’ walikwisha kuporomoshwa na wimbi la wakati – hatima ya kila binadamu. Soyinka haungi mkono mkabala wa Ngugi wa kuamua kimakusudi kuandika kazi zake za kiubunifu kwa lugha ya Kikikuyu badala ya Kiingereza.

Soyinka anadai kwamba fasihi yetu imekuwepo kwa lugha zetu za kiasili na fasihi andishi kwa lugha za kiasili inapatikana kotekote barani Afrika – sambamba na lugha za kigeni. Anasema kwamba kwa hakika, hapajakuwepo na uhaba wa ushairi, hadithi fupi na mitungo iliyoandikwa kwa lugha za kiasili.

Soyinka hana stahamala na waandishi wanaonadi vitabu vyao vilivyoandikwa kwa lugha za kiasili kwa madai ya kuutetea Uafrika.

Prof Wole Soyinka na Profesa Ali Mazrui ni marika – wote wawili walizaliwa 1934. Soyinka alizaliwa Abeokuta, Nigeria Magharibi huku Mazrui akizaliwa Mombasa, Kenya. Soyinka alilelewa katika mazingira ya Ukiristo huku Mazrui akilelewa katika Uislamu – baba yake alikuwa Kadhi Mkuu.

Ngugi wa Thiong’o alizaliwa 1938 katika familia ambayo haikuwa ya Kikiristo. Alielimishwa Alliance High School kabla ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza.

Prof Ochieng’ naye alisomea shule ya msingi ya Usenge kabla ya kujiunga na Alliance High School – Kikuyu, na baadaye Chuo Kikuu cha Nairobi alikojipatia shahada ya Uzamifu.

Soyinka ni mtunzi wa tamthilia, mashairi na riwaya. Mnamo 1986, Akademia ya Uswidi ilimtuza Tuzo ya Fasihi ya Nobel na kumtaja kuwa mmoja wa watunzi bora wa tamthilia kwa Kiingereza.

Mnamo 1986, kabla Soyinka kupokea Tuzo ya Fasihi ya Nobel, yeye (Soyinka) na Ngugi walitoma mihadhara katika Kongamano la Pili la Waandishi wa Kiafrika lililofanyika Stockholm, Uswidi. Soyinka alizungumzia mada ya ‘Maadili, Itikadi na Mhakiki’.

Aliwashambulia wahakiki wa fasihi ya Kiafrika ambao walikuwa wamembughudhi kwa mda mrefu. Ngugi kwa upande wake alizungumzia “Uandishi dhidi ya Ukolonimamboleo”.

Katika hotuba yake, Soyinka aliwashambulia wahakiki wa tungo zake wanaoibua fahiwa kwamba yeye huandika kuvutia hadhira ya wasomaji wazungu.

Alioneshwa kukerwa zaidi na wahakiki aliowafananisha na ndege aitwaye Chichidodo – katika riwaya ya Ayi Kwei Armah – The Beautiful Ones are Not Yet Born. Ndege huyu aitwaye chichidodo chambacho Ayi Kwei Armah hupiga kelele sana kuueleza ulimwengu jinsi anavyoyachukia mavi.

Kinaya ni kwamba, ndege huyu hula nini? Minyoo wanaoishi kwenye kinyesi cha binadamu. Kundi hili la wahakiki linadai kwamba Wole Soyinka, Christopher Okigbo na Michael Echeruo – ambao wote huandika kwa Kiingereza si waandishi wa kweli wa Kiafrika. Kisa na sababu? Wanautukuza uzungu.

Kundi hili la wahakiki ambalo lilimwandama Soyinka kivumbi kabla ya kushinda Tuzo ya Fasihi ya Nobel kuonesha jinsi angalivyohisi uchungu ikiwa asingeshinda tuzo hiyo.

Katika Decolonizing The Mind: The Politics of Language in African Literature, Ngugi anasema, “Kitabu hiki, naipa kwaheri lugha ya Kiingereza kama nyenzo ya uandishi wangu (wa kubuni). Kuanzia sasa kuendelea, nitakuwa nikiandika kwa kutumia Gikuyu na Kiswahili.”

[email protected]

Kwenye makala yangu, ‘Ngugi could do a lot more to promote Kiswahili in Kenya’ (Saturday Nation, Desemba 9, 2016), nilidai kwamba Ngugi amekisaliti Kiswahili.