Wakenya wakerwa na wabunge kulipiwa mamilioni kutazama fainali Urusi
Na WYCLIFFE MUIA
WAKENYA Alhamisi walieleza ghadhabu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuibuka kuwa wabunge 14 na maseneta sita wameenda Urusi kutazama mechi mbili zilizosalia za Kombe la Dunia.
Ilibainika kuwa waligharamiwa na walipa ushuru mamilioni ya pesa kwenda kufuatilia mchuano huo utakaoikutanisha Croatia na Ufaransa kwenye fainali hapo Julai 15.
Baadhi ya wabunge walioonekana wakijipiga picha maarufu kama ‘selfie’ wakiwa jiji kuu la Urusi, Moscow ni Seneta maalum wa Jubilee Millicent Omanga na Seneta wa Siaya James Orengo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Michezo Rashid Achesa, hakuna afisa wa michezo aliyehudhuria michuano hiyo kwa sababu wizara hiyo ‘haikuwa na fedha’.
Katika mahojiano na shirika la BBC, Bw Achesa alithibitisha kuwa serikali iliwalipia wabunge sita kwenda Moscow ili kujifunza ‘jinsi ya kuandaa mechi kubwa’.
Wakenya Alhamisi walitumia mitandao ya kijamii kuelezea ghadhabu zao kuhusu hatua ya bunge kutumia vibaya ushuru wao.
“Ni nini wabunge wa Kenya wanavuta? Inamaanisha serikali ilituma wabunge 20 ili waende kujifunza jinsi ya kuandaa mechi katika viwanja vya Bukhungu na Kamukunji? Tukiendelea hivyo hizi Ajenda Nne zitasalia ndoto ya mchana,” alisema @allen_arnold kupitia Twitter.
Naye @ConsumersKenya alisema: “Hawa wabunge ni sehemu tu ya sakata wanazoendelea kuchunguza. Nani ataokoa Wakenya? Waathiriwa wa Bwawa la Solai wanaendelea kuhangaika bila msaada huku Seneta (maalum) Millicent Omanga akipiga selfie mjini Moscow.”
Hata hivyo Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alitetea hatua hiyo akisema ni ‘ziara ya kawaida’ kwa wabunge.
Katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, Bw Muturi alisema serikali iligharamia ziara hiyo kwa sababu waliohudhuria ni wanachama wa Kamati ya Michezo na Utamaduni na wengine ni wa Bunge FC, ambayo ni timu ya kandanda ya wabunge.
“Ni kweli baadhi ya wabunge walisafiri Urusi kutazama Kombe la Dunia kama wanachama wa Kamati ya Michezo na Utamaduni na Bunge FC,” alisema Bw Muturi.