• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Jombi aaibisha demu aliyetaka warudiane

Jombi aaibisha demu aliyetaka warudiane

Na JOHN MUSYOKI

Embu Mjini

MWANADADA mmoja kutoka mjini hapa, alifokewa na kalameni kwa kujipendekeza kwake baada ya kumtema.

Inasemekana kwamba demu huyo alikuwa mpenzi wa jamaa huyo lakini wakaachana baada ya demu kukataa kuolewa naye.

Penyenye zinasema wakati huo demu alikuwa na kiburi na kusema hangeolewa na jamaa mwingine mwenye pesa.

Kalameni alipoona kitumbua chake kilikuwa tayari kimeingia mchanga, aliamua kuishi maisha ya ukapera huku akisubiri siku moja mola atamjalia.

Demu aliolewa lakini baada ya miezi tisa alishindwa kuvumilia maisha ya ndoa na akatengana na mume wake.

Kwa kuwa demu huyo alikuwa ameolewa na bwanyenye, alipora pesa nyingi na akaanza kujiendeleza kimaisha.

Majuzi, alikutana na jamaa na akaanza kujipendekeza akitaka warudiane lakini kalameni alikataa katakata ombi la mwanadada huyo.

“Pole sana mpenzi wangu. Nilikukosea sana na nimeamua turudianae ili tufungue upya ukurasa wa uhusiano wetu. Kwa sasa sina shida yoyote. Nilienda kutafuta pesa. Nina uwezo wa kugharamia mahitaji yako yote na pia yangu. Nakusihi unipe nafasi,” demu alisema.

Inasemekana ombi lake liliambulia patupu jamaa alipomgeukia na kumrushia maneno makali.

“Una nini sasa kama sio pesa za kupora. Mimi sio mjinga. Hapo awali ulipandwa na kiburi na kunitupa. Hata kama una mali kiasi gani hauna nafasi kwangu. Endelea kuponda raha tu. Pole sana. Ondoka mbele yangu, ” jamaa alimwambia demu.

Demu hakuwa na lingine ila kuondoka baada ya jamaa kukataa ombi lake. Baadhi wa watu walipigwa na butwaa baada ya jamaa huyo kufanya uamuzi ulioshtua watu wengi.

Hata hivyo, haikujulikana ikiwa baadaya Kalameni aliamua kusaka mke mwingine au alibadilisha msimamo wake huo mkali na kumkubali mkewe wa kwanza.

You can share this post!

KURUNZI YA PWANI: Thamani ya misitu ya Kaya kwa Mijikenda

Kipa aomba msamaha kwa kukubali kulimwa mabao 5

adminleo