Dondoo

Nusra kipusa afutwe kazi kukatalia chenji

July 18th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

Ruiru Mjini

Kidosho mmoja mhudumu wa baa mjini hapa nusra amwage unga alipofumaniwa na bosi akikataa kumrudishia mteja chenji yake.

Yasemekana mwanadada huyo aliajiriwa katika baa hiyo mwezi Aprili mwaka huu na alikuwa na mazoea ya kukosa kurejesha chenji ya wateja.

Juhudi za keshia kumuonya akomeshe tabia hiyo zilionekana kugonga mwamba.

Siku ya kisanga, mteja alimpa noti ya Sh500 atoe bili ya Sh450. Demu alilipa bili hiyo kwa keshia na akaweka chenji mfukoni.

Mteja alingoja chenji yake kwa muda wa dakika 20 hivi hadi akaamua kuuliza kipusa. “Bili yangu ilikuwa Sh450, na nimekupa Sh500 hivyo basi nangoja chenji ya Sh50,” jamaa alimfafanulia.

Inasemekana kipusa alijifanya hakusikia naye mteja hakuchoka kuitisha haki yake.

Kulingana na mdokezi, mteja alipoendelea kuitisha chenji, kidosho alimfokea akimweleza mwanamume hafai kungoja chenji kidogo kama hiyo.

“Wazee ninaowahudumia huwa hawangoji chenji ya pesa kidogo kiasi hicho. Hizi ni za macho kwa aliyekuhudumia,” alisema.

Wawili hao walirushiana maneno yasiyoweza kutajwa hapa. Ni katika harakati hizo ambapo mmiliki wa baa hiyo, ambaye ni mama alifika na kusikiliza malalamishi ya mteja.

“Wewe hizo tabia si katika baa yangu, nenda ufungue yako uwe ukibakia na chenji za wateja wako,” alichemka na kutisha kumpiga kalamu.

Inasemekana kipusa hakuwa na budi ila kumpa jamaa chenji yake ambaye alishukuru mmiliki wa baa hiyo kwa dhati.

Yasemekana mhudumu huyo alionywa na kutakiwa kuepuka tabia za aina hiyo ambazo bosi alizitaja kama za kumharibia biashara yake.