Kipusa afariki baada ya kuongezewa ukubwa wa makalio, daktari atoroka
Na AFP
RIO DE JANEIRO
DAKTARI mashuhuri wa kuongeza wanawake ukubwa wa makalio, Dkt Bumbum, ameenda mafichoni baada ya mteja wake kufariki.
Daktari huyo ambaye jina lake rasmi ni Denis Furtado husifiwa kuwa na uwezo wa kutenda ‘miujiza’ kwa miili ya wanawake, hasa makalio, na sifa zake zilienea kote nchini.
Lakini sasa amegeuka kuwa mhalifu anayesakwa na polisi baada ya mteja wake, kidosho Lilian Quezia Calixto, kufariki saa chache tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuongezwa ukubwa wa makalio yake.
Upasuaji huo ulifanywa nyumbani kwa Dkt Bumbum, katika mtaa wa kifahari wa Barra de Tijuca.
Calixto alikuwa amesafiri kilomita 2,000 kutoka nyumbani kwake Cuiaba kwenda kumwona daktari huyo lakini akaanza kuugua baada ya upasuaji.
Alipoenda hospitalini Jumapili, alikuwa akikumbwa na matatizo ya mpigo wa kasi wa moyo na shinikizo la damu.
Alipata mshtuko wa moyo mara nne kisha akafariki.
Punde baadaye, Furtado alitoweka na sasa polisi wanamsaka ili ashtakiwe kwa mauaji na kushiriki uhalifu. Mpenzi wake ambaye baadhi ya mashirika ya habari yanasema ni msaidizi wake, alikamatwa.
Chama cha Wapasuaji wa Urembo Brazil kiliharakisha kujitenga na Furtado na kumtaja kuwa mpasuaji bandia.
“Huwezi kufanya upasuaji ndani ya nyumba. Watu wengi wanahadaa wateja,” mkuu wa chama hicho Niveo Steffen akasema.
Imeripotiwa Furtado amewahi kushtakiwa mara nne kwa kufanya matibabu bila kibali na kutenda uhalifu wa wateja.
-Imekusanywa na Valentine Obara