• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Waathiriwa wa mafuriko Masinga wataka wafidiwe

Waathiriwa wa mafuriko Masinga wataka wafidiwe

Na CHARLES WASONGA

WAKAZI wa eneo bunge la Garsen wameitaka Serikali ya Kitaifa kuingilia kati na kuhakikisha kuwa kampuni ya Kuzalisha Kawi Nchini (KenGen) inawalipa ridhaa baada ya kampuni hiyo kufungulia maji ya bwawa la Masinga iliyowasababishia maafisa na uharibifu wa mali.

Wakiongozwa na Mbunge wao Ali Wario, wakazi hao Jumatano walielezea kwa machungu jinsi wapendwa wao saba walivyofariki katika maji ya mafuriko kando na kupoteza mifugo 1017.

Huku baadhi yao wakitiririkwa na machozi walilalama mbele ya wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kawi wakisema KenGen ilifungulia maji kutoka bwawa la Masinga, bila kuwapa notisi na ndipo yakawasababishia maafa.

“Mimi ni mmoja wa mwathiriwa wa tukio hilo. Nilipoteza mtoto wangu wa miezi minane na mtoto wa dadangu mwenye umri wa miaka 12. Wote wawili walikufa maji maji mnamo Mei 8, mwaka KenGen ilipofungulia maji bila kutupa notisi,” akasema Mzee Ibrahim Rufo huku akitokwa na machozi.

Yeye ni mkazi wa kijiji cha Galili, eneo la Tana Delta.

Akaongeza: “Mimi na mke wangu tulijaribu kuokoa kile ambacho tungeweza lakini kwa bahati mbaya tulipoteza mtoto na mali nyingi. Hatujapata mwili wa mtoto wangu mpaka sasa,”

Akielezea masaibu yake, mwathiriwa mwingine kwa jina Mohammed Golo, alilalama kuwa serikali haijakuwa ikishughulikia matatizo yao kama inavyofanya kuhusiana na janga la bwawa la Solai.

“Tunahisi kutelekezwa na serikali ilhali sisi ni Wakenya kama wale watu waliokumbwa na mkasa wa Solai na ambao walipata usaidizi wa haraka. KenGen ambayo imetuletea shida hii yote ni mali ya serikali,” akasema.

“Kiwango cha umasikini katika eneo bunge la Garsen na kaunti ya Tana River kwa ujumla imefikia kiwango cha asilimia 85. Hii ni kwa sababu ya kudorora kwa maendeleo katika eneo letu kunakosababishwa na maji haya,” Mzee Golo akaongeza.

Naye Mama Waithera Barji alielezea jinsi baadhi ya akina mama wenzake walifariki kufuatia kutopitika kwa barabara kutokana na maji ya mafuriko.

“Mama mmoja alifariki kwa sababu barabara ambayo ingetumiwa kumpeleka hospitali iliharibiwa na maji, Watoto pia wamekuwa wakipatwa na maradhi ya Pneumonia na upele huku wengi wao wakikosa kwenda shule kwa sababu shule zao zimeporomoka,” akasema mama huyo wa watoto wawili.

Bw Wario alisema kuwa kwa ujumla maji hayo yamesababisha hasara ya kima cha Sh701,820,000.

“Wakazi bado wanaendelea kupata hasara kwa sababu soko la Tana Delta limefungwa baada ya maradhi ya Homa ya Rift Valley kuzuka. Shule 12 zimefungwa na hatujui wakati ambapo zimesalia miezi mitatu kabla ya watoto kuanza mtihani wa kitaifa wa darasa na nane (KCPE),” akasema Mbunge huyo.

Mbunge huyo alisema kufikia sasa KenGen imewapa wakazi msaada wa bandili 200 pekee ya unga, akisema chakula hicho hakitoshi.

“Shirika la Msalaba Mwekundu (KRC) ndio wanatusaidia lakini wao pia wamelewa kwa sababu idadi ya wanaotaka msaada ni takriban watu 8,000,” akasema Wario.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Robert Pukose ambaye aliongoza kikao cha Jumatano, kwa niaba ya mwenyekiti David Gikaria, aliwahakikishia wakazi hao kwamba kamati hiyo itafanya kikao na KenGen.

“Shida zenu zimefikishwa kamati hii. Sasa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Serikali na KenGen wanashughulikia masaibu yenu,” akasema Dkt Pukose ambaye ni Mbunge wa Endebess.

You can share this post!

Mahakama kuamua iwapo itazuru bwawa la Patel

Seneti yatofautiana na serikali kuhusu kiini cha uchomaji...

adminleo