Matatu ya abiria 14 yanaswa ikibeba wanafunzi 31, wasichana na wavulana
Na CHARLES WANYORO
POLISI mjini Embu wamewakamata wahudumu wa matatu waliokuwa wakiwasafirisha wanafunzi 31 wa shule za upili kwa matatu ya abiria 14.
Wanafunzi hao kutoka Shule za Ikuu Girls na Ikuu Boys, Kaunti ya Tharaka-Nithi walikuwa wakielekea Nairobi kwa likizo ya Agosti mnamo Jumamosi.
Baada ya kufika mjini Runyenjes kwenye barabara ya Meru – Embu, matatu hiyo ilisimamishwa na polisi lakini dereva akakaidi na kutoroka. Kulingana na polisi, hawakulifuata gari hilo kwani walihisi kwamba huenda likaendeshwa kwa mwendo kasi, hali ambayo ingehatarisha maisha ya wanafunzi hao.
Polisi waliwasiliana na wenzao mjini Embu ambao waliweka kizuizi barabarani, hali iliyolazimu matatu hiyo kusimama.
Polisi walishangaa kuona idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa wamebebwa, huku wahudumu hao wakitoroka. Hata hivyo, walikamatwa na kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Embu, ambako gari hilo pia lilipelekwa.
Mkuu wa Polisi wa Embu Magharibi, Julius Meli alikataa kuzungumzia mashtaka ambayo watawafungulia wawili hao.
Baadaye polisi waliwasaidia wanafunzi kupata magari mengine na kuendelea na safari yao.
Kwingineko, utulivu umerejea katika mji wa Sololo, Kaunti ya Marsabit, baada ya taharuki iliyodumu kwa siku tatu kufuatia kukamatwa kwa mshukiwa wa ugaidi kijijini Manyatta Golbo.
Hali ya taharuki iliibuka baada ya shambulio dhidi ya msafara wa magari ya polisi ambayo yalikuwa yakisafirisha mshukiwa huyo mjini Moyale kutoka Kituo cha Polisi cha Sololo. Shambulio hilo lilifanyika katika eneo la Qate.
Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Sololo, Dennis Kieti alisema kuwa maafisa zaidi wa usalama walitumwa katika eneo hilo ili kuimarisha usalama. Vile vile, alithibitisha kwamba mshukiwa huyo alisafirishwa jijini Nairobi ili kuhojiwa zaidi.
Kulingana na Bw Kieti, mshukiwa alipatikana na bastola aina ya Ceska yenye risasi nane. Alisema kuwa wanashuku kuwa huenda ni mwanachama wa kundi la wanamgambo la Oromo Liberation Front (OLF) kutoka Ethiopia.
Mshukiwa alikamatwa na Kikosi Maalum cha Polisi wa Kukabiliana na Ugaidi (ATPU).
Tukio hilo lilizua taharuki, huku baadhi ya vijana wakiandamana kushinikiza kuachiliwa kwake.