• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Aliyemuua wakili kidosho kwa kukataa kumburudisha aona cha moto

Aliyemuua wakili kidosho kwa kukataa kumburudisha aona cha moto

Na RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kilabu cha kuuza pombe mtaani Buruburu kaunti ya Nairobi aliyemuua wakili mwenye umri wa miaka 27 baada ya kukataa wakienda kujivinjari alipatikana na hatia ya kuua akikusudia.

Erastus Ngura Odhiambo almaarufu Baba Billy alipatwa na hatia ya kumuua Linda Wanjiku Irungu na Jaji Stellah Mutuku aliyesema , “mshtakiwa alimzuia  marehemu kutoroka kisha akamvuruta kutoka ndani ya gari saa kumi unusu asubuhi kisha akampiga risasi begani na kumuua.”

Jaji Mutuku alisema mshtakiwa alikuwa mwenye hasira kali baada ya kumtafuta Wanjiku usiku wa Desemba 11, 2014.

“Mshtakiwa alikuwa amempigia simu bila kumpata mpenziwe. Alienda nyumbani kwake mara mbili na hakumpata. Alimpata mwendo wa saa kumi na nusu. Wanjiku alikuwa anajaribu kutoroka kwa gari lake mshtakiwa alipomsimamisha na kumtoa ndani . Walizozana huku  Linda akimtaka Odhiambo amwache,” Jaji Mutuku alisema.

Jaji huyo alisema mshtakiwa alitoa bastola kwenye mfuko wa nyuma wa suruali yake na kumpiga Wanjiku risasi katikla bega la kulia.

“Walinzi wawili waliokuwa wanalinda lango la makazi alipokuwa akiishi Wanjiku katika mtaa wa Buruburu Phase V  walishuhudia tukio hilo. Walimsikia Wanjiku akimwambia Odhiambo umenipiga risasi,” Jaji alisema akiongeza , “Mtaalamu wa upasuaji wa Serikali alitoa risasi kwenye kifua cha marehemu.”

Jaji Mutuku atamuhukumu Odiambo Julai 31 baada ya kiongozi wa mashtaka Bi Catherine Mwaniki kuwasilisha ripoti kutoka kwa familia ya Bi Wanjiku.

You can share this post!

Aliyeibia mamaye aponde raha na mchumba asukumwa ndani

Raha tele kwa kocha timu yake kuangusha Mathare

adminleo