Wakenya wa tabaka la chini kupumua bei ya umeme kushuka
Na VALENTINE OBARA
WAKENYA wanatazamiwa kunufaika kutokana na bei nafuu ya umeme kufuatia hatua ya Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) kutupilia mbali mapendekezo ya Kenya Power iliyotaka ada ziongozwe.
ERC Jumatatu ilifichua kuwa ilipokea pendekezo Januari kutoka kwa Kenya Power la kubadilisha bei ya umeme, ambapo miongoni mwa ada ilizopendekeza ziongezwe ni malipo ya kila mwezi ya Sh150 kwa wateja wa matumizi ya nyumbani, ambayo ilitakika iongezwe hadi Sh200.
Badala yake, ERC iliamua kuondoa ada hiyo ambayo wateja wote walikuwa wakilipia kila mwezi bila kujali kama wametumia umeme.
Ada hizo zilikuwa miongoni mwa zilizosababisha malalamishi mengi kutoka kwa wateja kuhusu gharama ya juu kupita kiasi ya umeme.
Mkurugenzi Mkuu wa ERC, Bw Pavel Oimeke, alieleza kuwa hatua iliyochukuliwa italeta usawa kwa kila mteja kwani watalipishwa kwa msingi wa kiwango cha umeme wanachotumia pekee.
“Hii imenuiwa kupunguza ada nyingi kwenye bili za umeme na kusaidia wateja kuelewa vizuri wanacholipia,” akasema, kwenye kikao cha wanahabari Nairobi.
Mbali na hayo, bei ya umeme imepunguzwa kutoka Sh17.77 kwa kila kilowati kwa saa, hadi Sh16.64. Malipo haya yatategemea kiwango cha umeme kinachotumiwa kwa mwezi
Kwa jumla, Bw Oimeke alisema bei ya umeme kwa matumizi ya nyumbani itapungua kwa asilimia 36.
Kwa upande mwingine, bei matumizi ya kibiashara na viwandani imepunguzwa kwa asilimia 4.4. Hii huenda ikasaidia kupunguza gharama ya uzalishaji bidhaa.
Kenya inatarajia kupanua uzalishaji wa umeme kutoka kwa mbinu nyingine kama vile upepo na mvuke ili kuongezea kiwango kinachozalishwa kutoka kwa nguvu za maji.
Miongoni mwao ni mradi wa uzalishaji umeme wa upepo katika Kaunti ya Marsabit na mradi wa uzalishaji umeme kutoka kwa mvuke katika eneo la Olkaria, Kaunti ya Nakuru.
Mnamo Mei, Benki ya Dunia ilionya kuwa bei ya juu ya umeme nchini ingehujumu malengo ya serikali ya kusambaza umeme kwa wananchi wote.
Ripoti yake iliorodhesha Kenya miongoni mwa mataifa ambapo umeme unasambazwa kwa kasi zaidi lakini gharama ya juu ni changamoto kubwa.
Bw Oimeke jana alisema kupunguzwa kwa bei hizo kutachangia zaidi kuimarisha maendeleo ya kitaifa hasa kupitia kwa utimizaji wa malengo manne makuu ya Serikali ya Jubilee kuhusu ustawishaji wa viwanda, uzalishaji wa lishe ya kutosheleza mahitaji ya wananchi wote, kuboresha huduma za afya na ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi.