Michezo

Gor yafungua mwanya wa alama 15 kileleni KPL

August 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA CECIL ODONGO

MABINGWA watetezi wa ligi ya KPL nchini Gor Mahia Jumatano waliendeleza udhabiti wao kileleni mwa ligi kwa kuwalisha Kariobangi Sharks kichapo cha 3-0  katika uga wa Moi mjini Kisumu katika mechi ya KPL.

Gor, ambao wametwaa ubingwa wa ligi mara 16, walipata mabao yao kupitia difenda wa Sharks Geoffrey Shiveka aliyejifunga mwenyewe katika dakika ya 25, Kevin ‘Ade’ Omondi dakika ya 76 kisha Brian Oketch aliyesajiliwa na K’Ogalo mapema mwaka huu kutoka Nzoia Sugar FC akatia msumari moto kwenye kidonda cha wapinzani kwa kufunga bao safi dakika ya 85.

Ingawa ‘Sirkal’ walitawala mechi nzima, Kariobangi Sharks mara kwa mara waliibuka tishio haswa kupitia wanadimba wao  Erick Kapaito na Harisson Mwendwa ambao waliwalazimisha walinzi wa Gor, Innocent Wafula na Harun Shakava kujituma na kuondoa mipira mingi ya hatari.

Aidha kipa Shabaan Odhonji alionyesha mchezo wa hali ya  juu langoni kwa kudaka na kupangua mipira hatari ikiwemo shuti kali kutoka kwa nahaodha wa Sharks, Bolton Omwenga katika dakika ya 70.

Kocha wa mabingwa hao Dylan Kerr alifanya mabadiliko makubwa kwa kikosi kilichocheza dhidi ya Yanga SC mjini Dar es Salaam Jumapili katika mechi ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho Barani Afrika CAFambayo walishinda 3-2.

Baadhi ya wanadimba waliotiwa kwenye kikosi cha kwanza ingawa mara nyingi wao husugua benchi ni kipa Shabaan Odhonji, madifenda Charles Momanyi na Bernard Ondiek, kiungo Cercidy Okeyo na mwenzake Lawrence Juma huku safu ya ushambulizi ikihimiliwa pakubwa  na limbukeni Boniface Omondi.

Walioanzishwa katika benchi  lakini wakaingia mechini kama wachezaji wa akiba kunogesha mtanange huo   walikuwa mfungaji Kevin Omondi, Wellington Ochieng’ na Joash Onyango.

Washambuliaji wazoefu Jacques Tuyisenge na George ‘Blackberry’ Odhiambo hawakuwa kikosini wala katika benchi ya kiufundi. Hali sawa na hiyo ilimkumba kipa Boniface Oluoch ambaye alilaumiwa majuzi  na wengi wa mashabiki kutokana na masihara mengi yanayomkumba  katika mechi mbalimbali ikiwemo mechi dhidi ya Yanga SC ambapo alifungwa mabao mawili rahisi kama kula pilau kwa kijiko.

Ushindi huo ulirejesha kumbukumbu za mchuano wa mkondo wa kwanza mapema mwaka huu ambao pia Gor Mahia  walishinda kwa idadi iyo hiyo ya mabao.

Kufuatia ushindi huo, K’Ogalo sasa wamefungua mwanya wa alama 15 kileleni mwa jedwali la ligi hiyo inayoshirikisha timu 18. Gor,  wamefikisha alama 55 huku nambari mbili Sofapaka waliolazwa mabao 2-1 siku ya Jumatatu  na Mabingwa wa mwaka 2012 Tusker wakifuata kwa alama 40.

Kariobangi Sharks bado wanasalia katika nafasi ya saba kwa alama 34

Vikosi katika mechi ya jana

Gor Mahia : Shaban Odhoji, Innocent Wafula, Harun Shakava, Charles Momanyi, Godfrey Walusimbi (Wellington Ochieng), Bernard Ondiek, Cercidy Okeyo (Kevin Omondi), Lawrence Juma, Francis Kahata, Ephrem Guikan (Joash Guikan) na Boniface Omondi.

Wachezaji wa akiba ambao hawakucheza

Peter Odhiambo, Wesley Onguso, Samwel Onyango, Raphael Asudi.

Kariobangi Sharks: Brian Bwire, Pascal Ogweno, Geofrey Shiveka, Bolton Omwenga, Michael Bodo Patilah Omoto Sven Yidah, Harrison Mwendwa ( Henry Juma.), Shaphan Oyugi ( Sydney Simale), Duke Abuya Eric Kapaito (Ebrima Sanneh)

Wachezaji wa akiba ambao hawakucheza

Gad Mathews, Francis Manoah, Wycliffe Otieno na Vincent Wasambo.