• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
LAMU: Mswada bungeni kufunga hoteli zinazoitisha vyeti vya ndoa

LAMU: Mswada bungeni kufunga hoteli zinazoitisha vyeti vya ndoa

NA KALUME KAZUNGU

MWAKILISHI wa Wadi ya Hongwe, James Komu anasema atawasilisha mswada katika Bunge la Kaunti ya Lamu hivi karibuni unaopendekeza kufungwa kwa hoteli zote za Lamu zitakazoitisha cheti cha ndoa ili kuwahudumia wateja wake.

Bw Komu anasema kamwe haridhishwi na tukio la mwezi jana ambapo hoteli moja mjini Kericho ilidinda kumhudumia Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Laikipi, Bi Catherine Waruguru baada ya kuwasili na mumewe kwa madai kwamba hawakuwa na cheti cha ndoa.

Komu anasema hatua hiyo ni ukandamizaji na haifai kuigwa na hoteli zingine zozote hapa nchini.

Alisema kuna haja ya wamiliki wa mahoteli kuheshimu haki na pia kuhifadhi siri za wateja wao iwe wake au waume.

Alisema hatua ya wamiliki wa mahoteli kuitisha cheti cha ndoa ili kuhudumia wateja wanaowasili kwenye hoteli zao ni sawa na kuanika siri za wateja hao.

Alisema haiwezekani wanaoingia hotelini kubeba cheti cha ndoa kana kwamba ni kitambulisho.

“Niko kwenye hatua za mwishomwisho kuandaa mswada nitakaowasilisha bungeni hivi karibuni kuhusiana na wenye mahoteli hapa Lamu. Kamwe sijafurahishwa na tukio la Kericho ambapo kiongozi alizuiliwa kuingia hotelini eti kwa sababu hana cheti cha ndoa.

Huo ni ukandamizaji wa haki za wateja. Mswada ninaoandaa  ukipitishwa utahakikisha hoteli zinazotaka cheti cha ndoa ili kuhudumia wateja wake hapa Lamu zinafungwa mara moja. Huwezi kubeba cheti cha ndoa kana kwamba ni kitambulisho ,” akasema Bw Komu.

Kauli ya Bw Komu aidha ilipingwa vikali na baadhi ya wakazi waliounga mkono sheria ya wanandoa kutoa stakabadhi ya kuwatambulisha kama wanandoa iwapo wanahitaji kuhudumiwa hotelini.

Bw Johnson Kamau anasema ni kupitia sheria hiyo ambapo itawafanya viongozi hasa wanasiasa kuheshimu ndoa zao.

Naye Bw Granton Hinzano, alisema kuitishwa kwa cheti cha ndoa kwa wale wanaoingia hotelini, hasa mke na mume kutasaidia kupunguza maovu yanayotekelezwa katika jamii.

“Tumejionea watu wa umri mkubwa wakishiriki ngono na wasichana wadogo kwa kujificha kwenye mahoteli.

Wabunge na viongozi wengine wamekuwa wakiwaficha wasichana wa vyuo vikuu na hata wanafunzi wa sekondari mahotelini na kuwatumia kama wapenzi. Sheria ya kuwasilisha cheti cha ndoa itapunguza maovu kama hayo kuendelea katika jamii zetu,” akasema Bw Hinzano.

You can share this post!

Kenya ilipoteza wasaa kushiriki mbio za mita 10,000 Nigeria

RAILA: Kwa nini simpendi Ruto

adminleo