Madiwani wa kike kuadhibiwa kwa kupigania dume
FRANCIS MUREITHI na MWANGI MUIRURI
Madiwani wawili wanawake wa Bunge la Kaunti ya Nakuru, huenda wakachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kupigana wakizozania mpenzi mmoja.
Inadaiwa kuwa wawili hao walipigana wakiwa katika mkahawa ulio ndani ya majengo ya Bunge la Kaunti hiyo mnamo Jumanne jioni.
Wawili hao waliripotiwa kubishana vikali kuhusu mapenzi kwa mwanamume mmoja ambaye ni diwani aliyechaguliwa katika bunge hilo kabla ya kuamua kurukiana wakararuriana nguo na kukwaruzana kwa makucha.
Jana, Taifa Leo ilifahamishwa kuwa suala hilo liliripotiwa kwa kamati ya nidhamu ya bunge hilo lichunguzwe.
Inasemekana kuwa wawili hao walibishana vikali wakiwa nje ya mkahawa huo huku wakirushiana matusi kabla ya kupigana. Walitenganishwa na walinzi wa bunge hilo na madiwani wengine wanawake.
Kaimu Spika wa bunge hilo Philip Wanjohi ambaye ni diwani wa wadi ya Lare alitaja suala hilo kwenye kikao cha madiwani na kusema ni ukiukaji wa kanuni za bunge.
“Huu ni ukiukaji wa kanuni za bunge. Tabia kama hiyo inadunisha hadhi ya bunge na haitakubaliwa,” Bw Wanjohi alieleza madiwani waliohudhuria kikao jana.
Alisema madiwani hao wawili walipaswa kusuluhusisha tofauti zao nje ya majengo ya bunge hilo. Afisa anayechunguza kisa hicho aliambia Taifa Leo kuwa wawili hao wanachunguzwa kwa kukiuka maadili ya uongozi kwa mujibu wa ibara ya sita ya Katiba.
Hata hivyo, kamanda wa polisi kaunti ya Nakuru Hassan Barua aliambia Taifa Leo kwa simu kuwa suala hilo linafaa kushughulikiwa na kamati ya nidhamu ya bunge la kaunti.Kulingana na Bw Barua, kisa hicho kilitendeka ndani ya majengo ya bunge ambapo madiwani huwa na kinga dhidi ya vitendo vyao.
“Suala hilo linapaswa kuchunguzwa na hatua za nidhamu kuchukuliwa na bunge la kaunti kwa sababu madiwani wana kinga dhidi ya vitendo vyao wakiwa ndani ya majengo ya bunge,” alisema Bw Barua.