Habari MsetoSiasa

Komeni kutumia bunge kulipiza visasi vya kisiasa, arai mbunge

August 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na FLORAH KOECH

MBUNGE wa Baringo Kaskazini, Bw William Cheptumo, ameomba wabunge wenzake wakome kutumia Bunge la Taifa kulipiza visasi vya kisiasa.

Mbunge huyo alisema kuna wabunge ambao wamekuwa na tabia ya kuingiza siasa bungeni badala ya kujadili masuala yanayohusu maendeleo.

Akizungumza wakati aliposimamia uzinduzi rasmi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi ya Kaimogol, Baringo Kaskazini, Bw Cheptumo alisema wabunge wanafaa kujadiliana kuhusu jinsi ya kuleta maendeleo kwa wananchi na wakome kupiga siasa bungeni.

Madarasa aliyozindua yalijengwa kwa ufadili wa Hazina ya Serikali Kuu ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NGCDF).

Alitoa mfano wa hoja ya Mbunge wa Kisumu ya Kati, Bw Fred Ouda, aliyetaka Naibu Rais William Ruto azuiliwe kuwania urais ifikapo mwaka wa 2022.

“Baadhi ya wabunge wamejishusha hadhi kwa kiwango cha kuleta hoja zisizo na msingi kikatiba. Kama wana malalamishi inafaa wayapeleke mahakamani badala ya kutaka kulipiza kisasi bungeni,” akasema.

Bw Cheptumo alisema Chama cha Jubilee kinalenga kuleta maendeleo kwa wananchi wala si kujihusisha kwa siasa za urithi za 2022.

“Katika chama chetu tunajihusisha na kutekeleza ahadi za maendeleo ya kiuchumi na wala si kupiga domo kuhusu nani anastahili zaidi kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ifikapo 2022. Bunge lina jukumu la kuangazia masuala muhimu kuhusu changamoto zinazokumba wananchi ambazo zinafaa kujadiliwa badala ya siasa za pesa nane ambazo haziwezi kutusaidia hivi sasa,” akasema.

Jumatano iliyopita, bunge lilitupilia mbali hoja iliyotaka kumzuia naibu rais kuwania urais 2022.

Hoja hiyo ya Bw Ouda ilitaka pia manaibu gavana waliohudumu kwa vipindi viwili wazuiliwe kuwania ugavana katika chaguzi zijazo kwa kuwa wao huchaguliwa pamoja na magavana.

“Uchaguzi wa rais na naibu wake ni moja. Wote wawili hutoa mamlaka yao moja kwa moja kwa wapigakura kwa hivyo wanastahili tu kuwa mamlakani kwa vipindi viwili visivyozidi miaka mitano kila kipindi,” sehemu ya hoja hiyo ikasema.

Lakini wabunge walikataa kuipeleka kwa kamati ya haki na masuala ya kikatiba inayosimamiwa na Bw Cheptumo licha ya juhudi za Spika Justin Muturi kutaka izingatiwe.