Habari Mseto

Mbunge apinga wazo la kuondoa shule za mabweni

August 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGATI OBEBO

MBUNGE wa Bomachoge Chache, Bw Alfa Miruka, amepinga pendekezo la kufutilia mbali shule za mabweni nchini.

Badala yake, mbunge huyo ametoa wito kuwe na mashauriano yatakayolenga kukabiliana na migomo ya mara kwa mara na uharibifu wa mali unaosababishwa na watoto wa shule za upili.

Bw Miruka alisema shule za bweni hutoa mandhari bora kwa wanafunzi kuendeleza masomo yao ikilinganishwa na shule za kutwa.

“Uchomaji wa mabweni shuleni haifai kuwa sababu ya kutosha kuanzisha mdahalo kuhusu kugeuza shule za mabweni kuwa za kutwa. Badala yake inafaa tuhimize wazazi kuhusu umuhimu wa kuwafanya watoto wao wawe wenye adabu njema kabla wajiunge na shule hizi,” akasema Bw Miruka.

Alhamisi iliyopita, Waziri wa Elimu Amina Mohamed, alisema pendekezo hilo litaamuliwa na wadau katika sekta ya elimu.

Waziri huyo alisema Kenya ni miongoni mwa mataifa machache katika ukanda huu ambayo bado hutumia shule za mabweni.

Jopokazi lililoundwa kuchunguza matukio ya migomo shuleni lilipendekeza kuwa baadhi ya shule za mabweni zigeuzwe kuwa za kutwa ili kukabiliana na utovu wa nidhamu katika shule hizo.

Bw Miruka alikuwa akizungumza katika Shule ya Upili ya St Edwards Nyabioto, eneo la Sengera katika eneobunge lake wakati wa hafla ya kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vyema katika masomo yao.

Alikabidhi basi la shule lililogharimu Sh6.9M kutoka kwa Hazina ya Serikali Kuu ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NGCDF) kwa shule hiyo.