• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
Polisi waliomuua mwanamke City Park nje kwa dhamana

Polisi waliomuua mwanamke City Park nje kwa dhamana

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wawili wa polisi wanaoshtakiwa kwa kumuua mwanamke katika bustani ya City Park, kaunti ya Nairobi waliachiliwa Jumatano kwa dhamana ya Sh700,000 pesa tasilimu kila mmoja

Akiwaachilia huru , Jaji Stellah Mutuku alisema upande wa mashtaka haukuwasilisha sababu za kutosha kuwezesha  korti kuwakataza dhamana.

Jaji Mutuku alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa na inaweza kutwaliwa tu “ wakati afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) imewasilisha sababu za kutosha  kuthibitisha kuwa washukiwa watavuruga kesi ama kuwatisha mashahidi.”

Jaji huyo alikubalia ombi la Konstebo William Kipkorir Chirchir na Konstebo Godfrey Kipng’etich Kirui  la kuchiliwa kwa dhamana akisema , “wamethibitisha kuwa watafika mahakamani kila wakati kesi inayowakabili itakapokuwa inasikizwa.”

Wawili hao wanakabiliwa na shtaka la kumuua Janet Wangui Wanjiku mnamo Mei 20 2018 katika bustani ya Citi Park akiwa ndani ya gari na mpenziwe.

Walikanusha shtaka dhidi yao walipofikishwa kortini mnamo Juni 11 mwaka huu na kuomba  waachiliwe kwa dhamana kupitia kwa wakili wao Bw Ham Langat.

Ombi hilo lilipingwa na kiongozi wa mashtaka Bi Catherine Mwaniki akisema , “ washtakiwa ni maafisa wa polisi na wako na uwezo wa kuwatisha mashahidi watakaofika kortini kutoa ushahidi dhidi yao.”

Pia alisema wawili hao watatoroka wakiachiliwa kwa dhamana kwa vile adhabu ya kesi inayowakabili ni kifo endapo watapatikana na hatia.

Bi Mwaniki alisema kuwa mumewe marehemu Bw  George Kirubi Gathima alipinga wawili hao wakiachiliwa kwa dhamana akidai, “amekuwa akipokea vitisho. Risasi kupigwa katika paa la nyumba mnamo Juni 17. Hoteli yake ijulikanayo Gloria Hotel kuchomwa mnamo Juni 23 2018 na gari lake kusukumwa na jingine katika barabara ya Jogoo.”

Bw Mwaniki alimsihi Jaji Mutuku awanyime washtakiwa dhamana akisema visa hivyo vyote dhidi ya Bw Gathima vinaashiria walihusika.

Bw Langat alipinga tetezi hizo na kumwuliza Jaji Mutuku , “Je, washtakiwa hawa walihusika aje na visa hivi vya vitisho dhidi ya mlalamishi (gathima ) na walikuwa rumande katika gereza kuu la Kamiti. Hawakuwa nje  ndipo watende hayo.”

Bw Langat alipinga ushahidi wa afisa anayechunguza kesi hiyo Konstebo Lawrence Irungu aliyesema amejaribu kushawishi  washtakiwa wafunguliwe mashtaka ya kuua bila ya kukusudia.

“Naomba hii mahakama iwaachilie kwa dhamana washtakiwa,” alirai Bw Langat.

Akitoa uamuzi , Jaji Mutuku , alisema ijapokuwa upande wa mashtaka umeeleza wasiwasi kuhusu washtakiwa kutoroka na kuvuruga mashahidi , hakuna ushahidi wa kutbitisha kwamba watachana mbuga wakiachilwa kwa dhamana.

Alisema kuwa washtakiwa ni maafisa wa polisi wanaoelewa athari za kutohudhuria vikao vya kesi.

Jaji Mutuku aliwaachilia kwa dhamana ya Sh700,000 pesa tasilimu na wakishindwa kuzipata wawasilishe mahakamani dhamana ya Sh2,000,000.

Pia aliwaamuru wasiwasiliane na mashahidi kwa njia yoyote ile. Aliagiza kesi hoyo itajwe mbele ya Jaji Jessie Leesit Septemba 19 itengewe siku nyingine ya kusikizwa badala ya siku ile ya Novemba 20-22, 2018.

Kuuawa kwa Bi Jane Wangui Waiyaki kulizua hisia kali huku miito ikitolewa na washika dau wahusika wakamatwe na kufunguliwa mashtaka.

  • Tags

You can share this post!

Wakurugenzi waliopunja Kenya Power Sh14.4m kutiwa nguvuni

Njama ya wanafunzi waliofeli KCSE kujipea ‘A’...

adminleo