Habari Mseto

Nzomo kuozea jela miaka 12 kwa kutwanga mkewe

August 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PIUS MAUNDU

DAUDI Nzomo, mwanaume aliyenaswa kwenye video akimshambulia mke wake, Winfred Mwende, kwa mangumi na mateke amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela.

Mahakama ya Makueni pia ilimhukumu Nzomo miaka mingine miwili nje ya mahakama ambapo atafanya kazi bila malipo katika taasisi za umma huku mienendo yake ikichunguzwa.

Video hiyo iliyokuwa ikisambazwa katika mitandao ya kijamii, inaonyesha Nzomo, 36, akimzaba makofi, magumi na mateke mke wake Bi Mwende huku watu waliokuwa karibu wakimsihi amwache.

Alikiri kutekeleza unyama huo Ijumaa iliyopita alipofikishwa mahakamani baada ya kukamatwa kijijini Nguu.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Makueni James Mwaniki alitoa hukumu hiyo baada ya kutathmini ripoti ya uhalifu ya mshtakiwa na kiwango cha majeraha aliyomsababishia mwathiriwa ambaye anaendelea kutibiwa jijini Nairobi.

Ripoti ya polisi iliyowasilishwa mahakamani na mwendesha mashtaka Bi Jenniffer Ndeda inaonyesha kuwa Nzomo amekuwa na mazoea ya kumpiga mkewe mara kwa mara.

Nzomo alimpiga Bi Mwende mnamo 2013 alipokataa mpango wake wa kuoa mwanamke mwingine. Hata hivyo, Nzomo baadaye alifanikiwa kuoa mke wa pili.

Nzomo ambaye anafanya kazi ya kusindikizia watu ng’ombe kutoka soko moja hadi jingine, amewahi kuuza mifugo wa mteja wake na kisha kutoweka na fedha, kulingana na ripoti.

Ripoti hiyo ilisema kesi dhidi ya Nzomo zimekuwa zikitatuliwa nje ya mahakama.

“Alijaribu kujitia kitanzi hivi majuzi akilalamika kuwa mkewe Mwende alikuwa na mpango wa kando,” Bi Ndeda akaambia mahakama.

Ripoti hiyo ilidhihirishia mahakama kuwa Nzomo alikuwa mtu mwenye fujo na hasira.

Nzomo, hata hivyo, alisihi mahakama kumsamehe huku akisema familia yake huenda ikaangaika endapo angepewa adhabu kali. “Ninaamini atatumia fursa hiyo gerezani kubadilika. Atakapokamilisha kifungo chake, tunatarajia kuwa atakuwa ameokoka na kwenda kanisani,” akasema Sammy Mbithuka, nduguye Nzomo.

Shirikisho la Mawakili Wanawake nchini (FIDA) lililotoa wakili kushughulikia kesi hiyo, lilipongeza adhabu hiyo.