• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Kaparo aondoka NCIC ukabila bado ukishamiri

Kaparo aondoka NCIC ukabila bado ukishamiri

Na PETER MBURU

KENYA ingali na kibarua kigumu kuwaunganisha raia wake ambao wamegawanywa na wanasiasa kwa misingi ya kikabila na historia ya tamaduni zisizokumbatia utofauti baina ya jamii.

Huu ndio ulikuwa ujumbe wa mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya amani na maridhiano (NCIC) Francis Ole Kaparo, katika hafla ya kukamilisha muhula wa kuhudumu wa makamishna wa tume hiyo katika hoteli ya Intercontinental jana.

Hatimaye makamishna wa tume hiyo jana waliondoka afisini, lakini ujumbe wa mwenyekiti wao ukawa wazi kwa taifa.

“Nimehudumia taifa hili katika ngazi tofauti; kama wakili, mbunge, waziri na spika wa bunge la taifa lakini hii ndiyo imekuwa kazi ya muhimu, ya dharura na ngumu kuliko zote.

Ngumu kwa kuwa Wakenya ni wakorofi na wanatafuta sababu za aina zote kupigana na kutofautiana, jambo linalofanya kuwaunganisha kuwa vigumu sana,” akasema Bw Kaparo.

Bw Kaparo alijutia kuwa japo angependa kurudi nyumbani kifua mbele, hali kwamba, bado kuna mengi yaliyosalia kufanyika ili kuwaleta Wakenya pamoja na kumaliza uhasama wa kikabila bado ni jambo linalofaa kutia hofu taifa hili.

“Ni bahati mbaya kuwa ninaondoka na siwezi kusema kwa ukweli kuwa hayo mambo yamekwisha. Ni jambo linalonipa masikitiko kuwa hatujawahi kukamilisha kazi ya kuwaleta Wakenya pamoja,” akasema Bw Kaparo.

Alitaja hali ya wanasiasa kuchochea utengano wa kikabila, ukosefu wa fedha za kuendesha shughuli za kukuza amani na ukorofi miongoni mwa wananchi kama baadhi ya matatizo makuu ambayo yamekwamisha utendakazi wa tume hiyo.

“Kazi ya kuwaleta Wakenya pamoja inaathiriwa na siasa na ukabila, watu wanaofanya kazi hii kuwa ngumu ni wanasiasa, ikiwa kweli tunataka kuwaleta Wakenya pamoja tuvunje ukabila, na kuvunja ukabila nchini kutaleta amani ya kweli,” Bw Kaparo akasema.

Hata hivyo, alisema tume hiyo imevuna matunda kwani kiwango cha amani nchini kimeinuka kuliko wakati wowote mwingine katika historia.

You can share this post!

Kaunti 13 zatuzwa na IMF kwa kutimiza viwango vya utendakazi

Serikali yatoa tahadhari mpya kuhusu Ebola

adminleo