Ni heri nipoteze marafiki nikiokoa Wakenya – Uhuru
JUMA NAMLOLA na IBRAHIM ORUKO
RAIS Uhuru Kenyatta amesisitiza kwamba vita dhidi ya ufisadi lazima viendelee, hata kama vitamfanya apoteze marafiki wa karibu.
Alisema, tayari baadhi ya marafiki zake wa muda mrefu wameanza kumtoroka, kwa kuwa amekataa kuwasaidia wasifikiwe na mkono wa sheria kwenye kampeni inayowalenga washukiwa wa ufisadi.
“Nimewapoteza marafiki wa karibu katika vita dhidi ya ufisadi. Lazima tuwe tayari kupoteza marafiki na kufanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu,” akasema katika kanisa la Faith Evangelistic Ministry (FEM) lililoko Karen, Nairobi.
Alieleza kuwa tangu ubomoaji wa majumba ya kifahari yaliyojengwa kwenye mikondo ya maji uanze, amekuwa akipokea simu kutoka kwa watu wakimtaka ausimamishe. Hata hivyo, aliapa kwamba lazima serikali imalize tabia ya watu kutojali sheria.
“Lazima tukabiliane na hali ya kutojali. Sio kwamba tunataka kubomoa majengo hayo bila sababu yoyote. Ikiwa hatutakabiliana na hali ya kutojali, basi hatutaafikia malengo yetu. Kwa nchi hii kufaulu, lazima tukabiliane na ufisadi na hali ya kutojali,” akasema Rais.
Akiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana katika kaunti ya Kisii, Rais Kenyatta aliwahimiza Wakenya wachukue jukumu la kuwakamata watu watakaopatikana wakiendeleza ufisadi.
“Nyinyi vijana, nataka muwakamate watu wote watakaohusika na ufisadi. Hata kama ni baba yako, afisa wa polisi, MCA au mbunge. Shikeni hao muwapeleke kwa polisi. Msiogope yeyote,” akasema.
Aliwataka wananchi wafahamu kuwa hakuna asiyeweza kukabiliwa na mkono wa sheria, iwapo atapatikana akijihusisha na ufisadi wa aina yoyote. Alisema hayo huku Usimamizi wa Bunge la Kitaifa ukilazimika kuchukua hatua kujiokoa na aibu ndogo ndogo za wabunge kupokea hongo ya hata Sh10,000.
Spika Justin Muturi Jumamosi alimwagiza Karani wa Bunge, Bw Michael salai awaandikie wabunge, ambao walionekana hadharani wakidai kuhongwa wiki jana, ili wakatae ripoti ya uchunguzi kuhusu sukari. Wabunge hao wanatakiwa wawasilishe madai yao kwa Kamati ya Bunge inayohusika na Mamlaka.
“Nimepata habari wabunge wameeleza hisia zao kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kuhusiana na yaliyojiri bungeni, muda mfupi kabla ya mjadala kuhusu ripoti ya sukari,”alisema Bw Muturi.
Aliongeza: “Afisi yangu na uongozi wa bunge kwa jumla tunachukulia madai haya kwa uzito unaostahili. Ni lazima uchunguzi wa kina ufanywe na hatua muafaka zichukuliwe.”
Jana, Bw Sialai alithibitisha kwamba kuanzia leo afisi yake itaanza kuwaandikia wabunge waliotoa madai kuhusu hongo wiki jana. Watakaoalikwa watatarajiwa kutoa maelezo yao kufikia Jumatano mchana.
Miongoni mwa wabunge wanaotarajiwa kutoa maelezo ni Bw Didmas Barasa (Kimilili) ambaye amekiri kuandamwa na mbunge wa kike aliyetaka kumpa Sh10,000. Wengine ni Simba Arati (Dagoreti Kusini), Justus Murunga (Matungu), Godfrey Odanga (Matayos), Tindi Mwale (Butere) na Ayub Savula (Lugari).