Dondoo

Mama mkwe amnyima jombi kiti eti ana kiburi

August 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na TOBBIE WEKESA

Luanda, Vihiga

KIOJA kilizuka hapa baada ya mama mkwe kuamrisha mume wa binti yake asipewe kiti cha kukalia. Hii ni baada ya polo kuhudhuria sherehe ya kulipa mahari ya mwanyumba wake. Inadaiwa mama mkwe alikuwa amekasirishwa na tabia ya polo ya kuwa na kiburi na kutomheshimu.

Kulingana na mdokezi, makalameni wote waliokuwa wameoa mabinti wa mama huyo walikuwa wamealikwa. Inasemekana polo ndiye aliyekuwa wa mwisho kuwasili.

Duru zinasema polo alipowasili, alimkuta mama mkwe akitoa shukrani zake kwa mabinti zake pamoja na waume wao kwa kuendelea kumsaidia.

“Huyu ni nani. Asipewe kiti mwanzo,” mama mkwe alifoka. Kila mtu alitulia na kushangaa. “Mimi sipendi watu wakaidi na wakora. Kiburi utampelekea mtu mwingine, si mimi,” mama mkwe alizidi kufoka.

Mabinti za mama huyo waliamua kuingilia kati ili kumtuliza mama yao. “Achaneni na mimi. Huyu jamaa hataketi hapa. Ana kiburi sana. Hana aibu hata kidogo kukanyaga nyayo zake kwenye ardhi yangu. Anataka nini,” mama aliwakaripia mabinti zake.

Kuona ameaibishwa, polo aliamua kumkemea mama mkwe.

“Acha zako. Kila wakati ukinipigia simu ni kuombaomba tu. Ni lini hata na wewe utatulia ufanye kazi,” polo alimfokea mama mkwe.Polo aliendelea kurusha cheche za matusi huku akiondoka karamuni.

“Hata kwangu kuna viti vya kuketi. Mwanzo si vya kukunjwa na vilivyojaa kunguni kama hivi vyako. Ni makochi kutoka Ulaya,” polo alifoka.

Mama mkwe alibaki mdomo wazi. Majirani walibaki kutazama sinema ya bure.

“Usiwahi kunipigia simu tena. Wale ng’ombe wawili niliokuletea wanakutosha,” polo alisikika akisema huku akienda.