'Hekima' ya Waititu kusongesha mito yashtua dunia
Na VALENTINE OBARA
GAVANA wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu, ameibua mjadala mkali nchini baada ya kupendekeza kwamba mikondo ya mito isongeshwe badala ya kubomoa majumba katika Kaunti ya Nairobi.
Kulingana na Bw Waititu, wawekezaji hutumia pesa nyingi katika ujenzi wa majumba hayo na ni makosa kwa serikali kubomoa bila kutilia maanani hasara inayosababishwa kwa wawekezaji.
Alisema jambo la busara litakuwa ni ‘kuhamisha’ mito au chemchemi za maji zilizoathirika, badala ya kutekeleza ubomoaji ambao umekuwa ukiendelea tangu wiki iliyopita.
“Kama kuna nyumba yako imekaribiana na mto, wewe uambiwe ni gharama yako kuhakikisha mto umesongea kidogo. Lakini kubomoa nyumba si suluhisho kusema kweli,” akasema.
Alitoa wito huo Jumapili alipohudhuria ibada katika kanisa lililoko eneo bunge la Kikuyu, ambayo pia ilihudhuriwa na Naibu Rais, Bw William Ruto.
Gavana huyo alitetea wawekezaji na kusema kwamba wengi wao waliponunua ardhi ambapo walijenga, hapakuwa na sheria iliyoeleza umbali unaostahili kujengewa kutoka kwa mito au chemchemi za maji.
“Msiende mbio kubomoa kwa sababu pengine mto ulikuwa umepita kwa ardhi iliyouzwa. Ilikuwa sehemu ya ardhi ya mtu mmoja aliyeinunua. Ubomoaji wa nyumba ni uchungu sana, watu waliwekeza pakubwa,” akasema, na kutoa wito kwa Bw Ruto aingilie kati suala hilo kwa vile anaelewa hali ya uwekezaji.
Wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii walimkosoa Bw Waititu na kusema pendekezo lake halijazingatia msingi wa ubomoaji unaoendelea, ingawa kuna wengine waliomtetea na kusema hafai kupuuzwa.
Mbali na hayo, Bw Waititu alitaka pia vita dhidi ya ufisadi viendeshwe polepole kwani kulingana naye, kuna hatari ya kuharibia watu majina ilhali huenda hakuna ushahidi wa kutosha kuwahukumu.
Ingawa kuna mataifa ambapo mikondo ya mito, bahari, ziwa au chemchemi zingine za maji huruhusiwa kubadilishwa ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa miundomsingi au majumba, sheria za Kenya huhitaji ujenzi ufanywe angalau mita 30 kutoka kwa maeneo hayo ya maji.
Kwa msingi huu, ujenzi wowote unaofanywa chini ya mita 30 kutoka sehemu ya maji huchukuliwa kama unyakuzi wa ardhi ya umma kwa njia inayosababisha uharibifu wa mazingira kwani imebainika wajenzi wengi hujenga bila kutoa nafasi kwa maji hayo kupita bila tatizo.
Wiki iliyopita, Taasisi ya Masoroveya ya Kenya (ISK) ilishauri serikali itafute mbinu nyingine ya kutatua suala la majengo yanayolengwa, ambayo idadi yao ni karibu 5,000.
Taasisi hiyo ilisema wawekezaji wengi walikuwa na stakabadhi za kuthibitisha walifuata kanuni zote wakapewa vibali vya kujenga katika maeneo hayo na hivyo basi kuna uwezekano wao kushtaki serikali katika siku zijazo.
Idara ya polisi pia ilitangaza kuwa imetenga sehemu maalumu kwa wawekezaji walio na malalamishi wakayawasilishe ili uchunguzi ufanywe.