Swazuri ang'olewa mamlakani NLC
Na CHARLES WASONGA
NAIBU mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa y Ardhi (NLC) Bi Abigael Mbagaya Mukolwe ameteuliwa kuwa kaimu mwenyekiti wa tume hiyo wakati ambapo mwenyekiti Mohammed Swazuri anakabiliwa na kesi mahakamani.
Profesa Swazuri alifikishwa mahakamani Jumatatu akikabiliwa na mashtaka ya ufisadi kuhusiana na ulipaji wa fidia kwa ardhi kulikojengwa reli ya kisasa (SGR) ya Sh221 milioni. Aliachiliwa huru kwa dhamana baada ya kusomewa mashtaka akiwa pamoja na afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo Tom Aziz Chavangi.
Kwenye taarifa kwa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumatano, NLC ilikana madai kuwa inakabiliwa na pengo ya uongozi kufuatia kushtakiwa kwa mwenyekiti pamoja na maafisa wengine, ikisema Bi Mukolwe ndiye sasa atatekeleza majukumu ya mwenyekiti.
“Tunajibu ripoti ambazo zimekuwa zikipeperushwa katika baadhi ya vyombo vya habari zikiashiria kuwa kuna mzozo wa uongozi katika tume kufuatia kushtakiwa kwa mwenyekiti Profesa Mohammad A. Swazuri na maafisa wengine,” ikasema taarifa hiyo iliyotumwa na mkurugenzi wa mawasiliano Bw Khalid M. Salim.
“Tume hii ingependa kusema kuwa uongozi wa tume uko imara kwani Naibu Mwenyekiti Abigael Mbagaya Mukolwe anatekeleza majukumu ya afisi ya mwenyekiti, jinsi ambavyo imekuwa ikifanyika mshikilia wa afisi akiwa nje ya afisi,” ikaongeza taarifa hiyo.
Naye Mkurugenzi wa habari za ardhi katika NLC David Kuria ndiye atahudumu kama kaimu afisa mkuu mtendaji.
Bw Benard Cherutich ambaye ni naibu mkurugenzi wa Fedha aliteuliwa kuwa kaimu mkurugenzi wa masuala ya fedha na usimamizi huku Bw Joash Oindo (Naibu Mkurugenzi wa utozaji ushuru na ukadiriaji thamani) atahuhudumu kama kaimu Mkurugenzo wa Ukadiriaji Thamani na utozaji kodi.
Wengine walioshtakiwa pamoja na Swazuri ni; Salome Munubi (Mkurugenzi wa Ukadiriaji Thamani na Utozaji Ushuri), Francis Karimu Mugo (Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha na Usimamizi.
Wote walikana madai na kuachiliwa huru kwa dhamana ya Sh3.5 milioni kila mmoja. Kesi hiyo itasikizwa kwa mara ya kwanza mnamo Agosti 29, 2018.
Kando na hayo, Hakimu Mkuu Lawrence Mugambi aliamuru kwamba washukiwa wote waliwasilisha stakabadhi zao za usafiri mahakamani.
Maafisa hao wa NLC hawataruhusiwa kwenda kazini hadi kesi inayowakabilia itakaposikizwa na kuamuliwa.
Swazuri alishtakiwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Nchini (KR) Atanas Maina kwa kushirikiana kulipa ridhaa zaidi ya Sh221 milioni kama ridhaa kwa ardhi ya shirika hilo ambayo ilinyakuliwa na watu na kampuni mbalimbali.