• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 1:35 PM
Gavana Awiti akana uvumi analenga kujiuzulu

Gavana Awiti akana uvumi analenga kujiuzulu

Na BARACK ODUOR

GAVANA Cyprian Awiti wa Homa Bay amekanusha kuwa anapanga kujiuzulu baada ya Mahakama ya Rufaa kusisitiza kwamba hakuchaguliwa kihalali.

Jana, gavana huyo alirejelea majukumu yake ya kawaida baada ya kukosekana kwa muda wa miezi miwili kwa kuugua. Kesi dhidi yake iliwasilishwa na mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi wa Agosti 8, Oyugi Magwanga.

Na licha ya uamuzi huo, Mahakama ya Juu imemruhusu kuendelea kuhudumu, kwanio kesi kuhusu uhalali wa uwepo wake afisini ingali kuamuliwa.

Na anapoendelea kupigania kiti chake, kuliibuka madai kwamba aliamua kujiuzulu kwa msingi kuwa aliogopa kushindwa tena katika kesi hiyo. Hata hivyo, amekanusha madai hayo.

“Sipangi kujiuzulu kutokana na kesi zinazonikabili. Ninaendelea na majukumu yangu kama kawaida,” akasema Bw Awiti.

Kiongozi huyo alisema upasuajiwa jicho lake ulifaulu baada ya kulazwa hospitalini.

“Madaktari wangu walinishauri kupumzika kwa muda baada ya matibabu,” akasema Bw Awiti.

Kwa sasa, ameagiza mawaziri wote na wakuu wa idara kumweleza mikakati ya kimaendeleo wanayoendeleza.

“Lazima idara zote zinionyeshe mikakati zinayoendeleza ili kuimarisha maisha ya wakazi,” akasema. Alielezea kuhusu miradi ya maendeleo ambayo kaunti yake inalenga kuhitimisha katika miezi michache ijayo.

Akiwahutubia wanahabari afisini mwake, alisema kuwa haogopi hatima ya kesi zinazomkabili.

Kikao hicho kilikuwa cha kwanza tangu Mahakama ya Rufaa kuunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu kufutilia mbali kuchaguliwa kwake.

“Nimekuwa nikiheshimu maamuzi ya mahakama. Nitafanya vivyo hivyo. Lengo langu ni kutimiza ahadi nilizotoa kwa wakazi” akasema Bw Awiti.

Kwa miezi hiyo miwili, Naibu Gavana Hamilton Orata na Katibu wa Kaunti Isaiah Ogwe ndio wamekuwa wakisimamia shughuli muhimu za serikali yake.

You can share this post!

Kivuko cha Likoni sasa kuwekwa CCTV

TAHARIRI: Kinaya ni kuwa hela za ushuru bado zitafujwa

adminleo