Michezo

TZ yaimumunya Sudan kama pipi U-17

August 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Geoffrey Anene

WENYEJI Tanzania wametinga nusu-fainali ya soka ya Afrika Mashariki na Kati ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika la Under-17 mwaka 2019 baada ya kulima Sudan 5-0 jijini Dar es Salaam, Alhamisi.

Alistides Agiri Ngoda na Kelvin Paul wamefungia Tanzania mabao mawili kila mmoja katika ushindi huo mnono kwenye mashindano haya ya mataifa tisa.

Tanzania, ambayo itaandaa AFCON U/17 mwaka ujao, ilipata bao la ufunguzi kutoka mchezaji ambaye si wake Omar Yousif Khamis Miso. Msudan huyu alitikiza nyavu zake akijaribu kuondosha hatari dakika ya 19 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Paul alipata mabao yake mapema katika kipindi cha pili kabla ya mabao zaidi kupatika kupitia kwa Ngoda.

Paul na Ngoda walifungia Tanzania ilipocharaza Burundi 2-1 katika mechi yake ya ufunguzi Agosti 11. Baada ya ushindi huu mkubwa kushuhudiwa kwenye mashindano haya tangu yaanze Agosti 11, Tanzania imerukia juu ya jedwali la Kundi A kwa alama sita. Rwanda pia imefuzu kushiriki nusu-fainali baada ya kupapura Sudan 3-1 na Burundi 4-3 katika mechi zake mbili za kwanza.

Kenya imesakata mechi moja katika Kundi B. Vijana wa kocha Michael Amenga wana alama tatu kutokana na ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Sudan Kusini 4-0. Watarejea ulingoni kuzichapa dhidi ya Djibouti hapo Agosti 17. Ethiopia inaongoza kundi hili kwa alama sita baada ya kushinda Uganda 1-0 na Djibouti 4-0.

Matokeo na ratiba:

Kundi A

Rwanda 3-1 Sudan (Agosti 11)

Tanzania 2-1 Burundi (Agosti 11)

Burundi 3-4 Rwanda (Agosti 13)

Sudan 0-5 Tanzania (Agosti 16)

Burundi na Sudan (Agosti 18)

Rwanda na Tanzania (Agosti 21)

Kundi B

Sudan Kusini 2-1 Djibouti (Agosti 12)

Uganda 0-1 Ethiopia (Agosti 12)

Kenya 4-0 Sudan Kusini (Agosti 14)

Djibouti 0-4 Ethiopia (Agosti 14)

Sudan Kusini na Uganda (Agosti 17)

Djibouti na Kenya (5.00pm, Agosti 17)

Djibouti na Ethiopia (Agosti 19)

Kenya na Uganda (5.00pm, Agosti 19)

Uganda na Djibouti (Agosti 22)

Ethiopia na Kenya (5.00pm, Agosti 22)