Gor sasa yahitaji alama 5 pekee kutetea ubingwa
Na GEOFFREY ANENE
MABINGWA watetezi Gor Mahia watahifadhi taji wakipata alama tano kutoka mechi zao nane zilizosalia kwenye Ligi Kuu ya msimu 2018 baada ya kubwaga Chemelil Sugar 1-0 uwanjani Moi mjini Kisumu, Alhamisi.
Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, Eliud Ekadeli Lokuwam, ambaye alisajiliwa na Gor mwaka 2017, alifungia waajiri wake bao la ushindi dakika ya 76.
Mvamizi huyu kutoka kaunti ya Turkana alijaza nafasi ya Samuel Onyango dakika ya 66. Ilimchukua dakika 10 pekee uwanjani kuleta tofauti katika mchuano huu baada ya safu ya ulinzi ya Chemelil kukosa kuondosha hatari ndani ya kisanduku.
Gor, ambayo inanolewa na kocha Muingereza Dylan Kerr, sasa ina alama 65 kutokana na ushindi 20, sare tano na kichapo kimoja.
Mabingwa hawa mara 16 wako alama 17 mbele ya wapinzani wake wa karibu Bandari, ambao wamesakata mechi moja zaidi. Mara ya mwisho Gor walilemewa na Chemelil ilikuwa 3-0 Machi 28 mwaka 2010.
Gor itakuwa ugenini dhidi ya mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka katika mechi yake ijayo hapo Agosti 22. Sofapaka inashikilia nafasi ya nne kwa alama 43 kutokana na mechi 26.
Wakishinda Sofapaka na kulima mahisimu wao wa tangu jadi AFC Leopards mnamo Agosti 25, watatawazwa mabingwa wa ligi hii ya klabu 18. Leopards, ambayo inaongozwa na kocha kutoka Argentina Rodolfo Zapata, inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 45 kutokana na mechi 26.