Telkom sasa yazindua maeneo 200 yenye mawimbi ya 4G
Na BERNARDINE MUTANU
SAFARICOM inakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Telkom Kenya baada ya kampuni hiyo kuzindua maeneo 200 yaliyo na mawimbi ya 4G, Nairobi.
Kampuni hiyo inalenga kuwavutia wakazi wengi zaidi wa Nairobi katika mtandao wake kwa kuongeza kasi ya mawimbi yake ya Intaneti.
Kwa kuongeza maeneo yaliyo na mawimbi ya 4G, mtandao wa Telkom utaongeza maeneo ambako unapatikana kutoka asilimia 15 hadi 55.
Hatua hiyo imeongeza idadi ya maeneo yaliyo na mawimbi hayo Nairobi hadi 300.
“Lengo letu kuu ni kujenga mfumo dhabiti ambao unatoa mawimbi yaliyo na kasi na kukuza uwezo zaidi pamoja na kuboresha huduma,” alisema afisa mkuu wa teknolojia w Telkom Kenya John Barorot.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo pia inalenga kueneza mawimbi yake kwingineko na kuifanya kuwa inaweza kutegemewa.