Wawakilishi Wanawake sasa wamulikwa kuhusu mabilioni waliyopewa
Na BERNARDINE MUTANU
WAWAKILISHI Wanawake wamemulikwa na mchunguzi wa matumizi ya fedha za serikali Edward Ouko kuhusiana na matumizi ya Sh4 bilioni walizopewa.
Katika ripoti yake ya mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 2017, alizua maswali kuhusiana na matumizi ya Sh4,013,958,103 ambazo alisema kamati za kaunti zimekataa kutoa stakabadhi zinazoonyesha matumizi yake.
“Ripoti za kamati za kaunti kuhusu miradi hazikutolewa kwa uchunguzi. Hakuna stakabadhi zinazoweza kutumiwa kuthibitisha kuwa malipo yalitolewa,” ilisema ripoti hiyo.
Hivyo, Bw Ouko hajaweza kuchunguza matumizi ya fedha hizo kuidhinisha ikiwa ziliharibiwa au zilitumiwa ipasavyo kuambatana na kanuni.
Pia, mchunguzi huyo aliibua maswali kuhusiana na matumizi ya Sh123 milioni za hazina ya dharura, ambazo hazikuweza kufuatiliwa.