WATOTO: Mkali wa nyimbo anayesisimua kwa weledi wake
Na PATRICK KILAVUKA
UBUNIFU na kujitolea katika kukuza vipawa vyake, kulimweka katika hali ya kutimiza ndoto yake ya kuwa kiongozi wa nyimbo, mwigizaji, msakataji densi, mtunzi na mwimbaji.
Ueledi wake umemwezesha kuongoza kikundi cha kusakata densi cha shule anakosomea na kupeperusha bendera ya Kanda ya Nairobi katika mashindano ya kitaifa ya Tamasha za Muziki Kenya kitengo cha shule za msingi (KMF) mwaka huu ambazo zitakuwa Kaunti ya Nyeri mwezi ujao.
Hata hivyo, mwaka jana pia alikifikisha kikosi cha shule hiyo katika mashindano hayo na kuibuka ya tatu bora kitaifa akiwa anaongoza wasilisho la densi ya kigirima yenye kichwa Sengenya (inachezwa wakati wa sherehe za furaha). Alitajwa kiongozi bora wa nyimbo na wa kupigwa mfano.
Mashindano hayo yaliandaliwa Kaunti ya Kakamega.
Monica Akinyi,13, ni mwanafunzi wa darasa la nane shule ya Msingi ya Marura, Kariobangi, Kaunti ya Kasarani. Usisahau shule hiyo ndiyo mwanafunzi mkongwe zaidi marehemu Stanely Murage alisomea baada ya kuhamia Nairobi baada ya ghasia za vita ya uchaguzi.
Msanii huyu chipukizi alianza kuonesha uwezo wa talanta yake akiwa mshiriki wa kanisa la Umoja SDA alikopata malezi ya kipawa chake cha usanii chini ya mwalimu wake Celestine Kwamboka na kikaota mizizi.
“Ninakumbuka tukishiriki katika mashindano ya makanisa yetu na nikashinda Ksh 12,000 na kupewa cheti. Mashindano hayo yaliandaliwa katika kanisa la Kwa Reuben na niliona hiyo kama kichocheo kikuu cha kipawa changu ambacho kinachangia ufanisi wangu.
Isitoshe, shuleni mwaka 2016, mwalimu Pauline Onyango alinitambua kuwa na talanta adimu na akanichonga zaidi,” anadokeza Akinyi ambaye amebeba jina la shule kwa miaka miwili mtawalia 2017 na mwaka huu akiongoza kikosi cha wanadensi waimbaji kuibuka wa tatu bora kitaifa mwaka 2017.
Alifuzu tena kushiriki makala ya kitaifa ya mwaka huu baada ya kuibuka kidedea katika mashindano ya Kanda ya Nairobi na kupokea mwenge wa kuiwakilisha wakiwa na wasilisho la densi ya wagirima yenye mada Gonda (Mwaliko) daraja ya 817H.
Mashindano ya Kanda ya Nairobi yaliandaliwa Shule ya msingi ya Westlands, juzi. Kufika kiwango cha Kanda, alikuwa amewaongoza wanadensi wa shule hii kuibuka wa kwanza bora katika mashindano ya kaunti ndogo ya Kasarani.
Akinyi anaongoza kikosi cha wasanii 24- wavulana 11 na wasichana 13 ambacho kina waimbaji na wasakataji densi pamoja na wachezaji ala.
Na ni vipi mwalimu alimteua kuwa kiongozi wa nyimbo?
Mwalimu Pauline anasema alimtambua baada kuwafanyia majaribio ya vipawa na hapo ndipo aligundua kwamba, ana sauti ya ninga au mwororo akiimba, ana uwezo wa kuchezea densi kwa urahisi, ni mjasiri, anajiamini na mkakamavu akiwa anaimba kisha akaanza kumnoa na kukuza kikundi kizima.
Huwafanyisha mazoezi kabla ya saa mbili asubuhi na kati ya saa kumi na saa kumi na moja.
Ingawa hivyo, Akinyi anasema yeye hujiongezea ncha ya maarifa kupitia mazoezi ya ziada akiwa nyumbani baada ya kufanya kazi za nyumbani na kazi za ziada za masomo hali ambayo inamweka katika nafasi bora kuwianisha masomo yake na talanta zake.
Fauka ya hayo, angependa kuwa daktari wa upasuaji na anayatilia maanani masomo ya Hesabu, Sayansi na Kiingereza kutimiza ndoto hiyo.
Usanii wake umeiva kwani amefinyangwa hadi anaweza hata kujitunga nyimbo zake haswa za injili ambazo anatazamia kuzirekodi pindi tu atakapopata mtaji au ufadhili zikiwa Peace( aliutunga wakati wa uchaguzi kuhimiza udumishaji amani), Wanadamu, Ping Oruno, Wana were na Tubebe Mizigo.
Yeye pia ni mwigizaji na msakatji densi shueni na kanisani. Manufaa ya Vipawa vyake?
Anasema vimemwezesha kutambuliwa, kuinua jina la shule na kuliweka kwenye ramani ya mashindano ya sanaa, kujigundua zaidi kitalanta na kutalii sehemu zingine nchini.
Uraibu wake ni kuimba na kusakata densi.
Mwisho anawahimiza wazazi kukuza talanta za wanao pasi na kuzificha ili zitiwe moto zaidi na kufufuliwa.