• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
WATOTO: Usogora wake wa kupiga ngoma wanogesha tamasha

WATOTO: Usogora wake wa kupiga ngoma wanogesha tamasha

Na PATRICK KILAVUKA

Kufinyanga kipaji kunahitaji uwe mwenye kuchochea, nia, mazoezi, bidii ya mchwa, nidhamu, kukikuza na kukubali marekebisho ndiposa ukikisimike kwenye mwamba usiotikiswa.

Isitoshe, uwe na ufahamu na kukabili changamoto ambazo huibuka katika safari ya kukikuza kwani kila barabara ina kona yake ila, aliye safirini ndiye anayetambua kwa kupitia ndiposa atue nanga vyema safarini pasipo na mawaa.

Mchezaji ala stadi Peter Maundu akipia ngoma wakati wa mazoezi kabla kushiriki katika Tamasha za Muziki Kenya za Kanda ya Nairobi ambazo ziliandaliwa Shule ya Msingi ya Westlands. Picha/ Patrick Kilavuka

Kauli hii ilitolewa na mchezaji magoma Peter Maundu, 14, mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi ya Light House Grace Academy, Riruta ambaye chini ya mwaka mmoja amejitahidi kuimarisha kipawa chake na mwaka huu, ameichezea ala shule yake kwa ueledi mkubwa hadi sasa ambapo inaenda kushiriki mashindano ya kitaifa ya Tamasha za Muziki Kenya baada ya shule kuibuka ya pili bora katika Kanda ya Nairobi chini ya uelekezi wa mwalimu Patrick Agunda. Mashindano yanaandaliwa Kaunti ya Nyeri wiki ijayo.

Ukungutaji wake uliunogesha wimbo wao katika mashindano hayo katika daraja ya 246 wakiwasilisha wasilisho lenye kichwa Tukomeshe Ukabila.

Wimbo huo wa tarabu unapiga kumbo athari ya mbegu hii katika taifa.

Kikosi cha nyimbo kikicheza densi Taarab. Picha/ Patrick Kilavuka

Ingawa alifanya mazoezi kwa miezi sita tu kuimarisha uwezo wake wa kuwianisha biti za wimbo na muambatano wa sauti za waimbaji, jopo la wakaguzi liliusifia uchezaji wake kuwa bora kutokana na vile ulikoleza katika wimbo hali ambayo iliwapelekea kuibuka wa pili bora katika kategoria hii na alama 86 nyuma ya Karura Forest ambayo ilibuka ya kwanza na asilimia 87 katika mashindano ya Kanda ya Nairobi ambayo yaliandaliwa Shule ya Westlands japo katika ya Kaunti Ndogo ya Dagorreti ambayo yalifanyika Shule ya Msingi ya Kinyanjui, waliibuka kidedea na alama 80.

Kupitia mashindano hayo anasema talanta yake imejitokeza zaidi na amejizolea maarifa mengine baada ya kukutana na wachezaji ala kutoka tamaduni tofuati.

Aonyesha weledi wake katika uchzeaji wa ngoma. Picha/ Patrick Kilavuka

Maundu alianza kuwa na kiu na nia ya kucheza ala tangu akiwa mtoto kwani, alizoea kupigapiga vitu ambavyo aliamini vinaweza kutoa sauti. Hata shuleni ilikuwa ada kwake kupigapiga dawati ili itoe mdundo. Hali hii iliwapelekea wanafunzi wengine kulalama kuhusu hilo japo hakukata tamaa kwani, yeye alijua fika ni msukumo wa talanta yake.

“Kipaji kikijitokeza huwa hakizuiliki! Msukumo ndani ya msanii mhusika humpelekea kuwa na kusudio la kukidhihirisha. Hali hii ilikuwa inanisukuma kucheza dawati kama njia ya kujichangamusha na kujichochea,” anadokeza Maundu ambaye hufanya mazoezi yake ya kucheza vyombo kila baada ya masomo, wikendi na hujiongezea maarifa kwa kucheza katika kanisa la Light House Grace, Riruta na ile ya kanisa la KAG, Nakuru akiwa nyumbani.

Wakikariri ngonjera la Tukomesha Ukabila wakiongozwa na kiongozi wa nyimbo huku Maundu akicheza ala. Picha/ Patrick Kilavuka

 

Msanii huyu chipukizi ana matamanio ya kuwa mchezaji wa kimataifa na hata kuwachezea wasanii wakati wa kunasa miziki.

Katika masomo anasema anapenda masomo ya Sanyansi Hesabu, Jamii na Kiswahili huku uraibu wake ni kusikiza muziki.

Wakionyesha miondoko ya taarabu wakicheza densi. Picha/ Patrick Kilavuka

You can share this post!

DAGORETTI: Mabingwa wa soka shule za upili Nairobi

Oduor aomba Mathare walaze Nakumatt wapande nafasi ya 4 KPL

adminleo