Habari Mseto

Ajabu ya magari ya serikali kupigwa mnada kwa Sh32,000!

August 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

WIZARA ya Leba imejipata matatani kufuatia mnada wa magari ya kifahari yanayomilikiwa na serikali kwa bei ya chini sana.

Baadhi ya magari yaliuzwa kwa Sh32,000 na kushtua wananchi. Wizara hiyo ilishutumiwa kwa kuficha mnada wa magari 17 baada ya kuweka tangazo kuhusu uuzaji wa magari hayo Aprili 7, 2017 katika gazeti moja la kitaifa badala ya magazeti mawili kuambatana na kanuni.

Mchunguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko alisema magari hayo 17 yakiwemo Volkswagen Passat na Nissan Patrol, yote yaliuzwa kwa kwa bei ya jumla ya Sh1.1 milioni.

Bw Ouko amependekeza hatua kali kuchukuliwa dhidi ya maafisa wa serikali, kampuni iliyonadi magari hayo na wahusika wengine ambao walihusika katika kisa hicho.

Kulingana na Ouko, ingawa magari hayo yalitathminiwa na bei yake kuwekwa na Wizara ya Uchukuzi, magari hayo yaliuzwa kwa bei ya chini sana.

Baadhi yake yaliuzwa hata chini zaidi ya bei ya mnada na mengine yalionekana kuvutia ‘bei za ajabu.’