Makala

KURUNZI YA PWANI: Wakazi kupata shule ya kisasa

August 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na KAZUNGU SAMUEL

UNAPOFIKA katika kijiji cha Zia Ra Wimbi, eneo bunge la Ganze, utalakiwa na jengo moja refu lililochakaa. Jengo hili limekuwa shule ya wakazi wa kijiji hiki kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Na licha ya ubovu wake, tulikutana na watoto wakiendelea na masomo yao, kudhihirisha ari ya kuitafuta elimu ambayo imewajaa.

Hata hivyo, sasa kuna matumaini kwani ubalozi wa Afrika Kusini ukishirikiana na mashirika mbalimbali ya nchi hiyo uliamua kufadhili ujenzi wa madarasa manne ya kisasa.

Hii ni baada ya ziara iliyofanywa na mbunge wa eneo hilo Teddy Mwambire hadi katika afisi za ubalozi huo jijini Nairobi kuomba msaada.

Na tulipofika katika eneo ambalo shule hiyo mpya inajengwa, wanakamati walikuwa wakikagua shughuli hiyo ambayo waliita kama mwanzo mpya kwa wakazi wa Zia Ra Wimbi.

Katika ziara hiyo, tuliandamana pia na mbunge huyo ambaye alisema kuwa shule hiyo mpya itabadilisha mtazamo wa elimu katika kijiji hicho.

Mwenyekiti wa shule hiyo Bw Kazungu Kiponda alisema kuwa siku moja walipata wafadhili ambao waliletwa na mbunge huyo.

“Sisi hata hatukuwa na habari lakini mbunge alikuja siku moja na kusema kwamba kulikuwa na wafadhili ambao walitaka kusaidia kujenga shule hii.

Baada ya mwezi mmoja wafadhili kutoka ubalozi wa Afrika Kusini walifika hapa na kutuahidi majengo,” akasema Bw Kiponda.

Kulingana na mwenyekiti huyo, shule zinazokaribiana na kijiji hiki ziko mbalimbali na hilo limekuwa likiwatesa sana watoto kutafuta elimu.

“Shule zinazopakana na kijiji hiki cha Zia Ra Wimbi ziko mbalimbali sana. Shule hizo jirani ni Palakumi, Mabathani, Lwandani na Kirimani. Lakini ziko mbalimbali sana,” akasema Bw Kiponda kabla ya kuongeza “Shule hii mpya itafanya wazazi kuwaleta watoto wao hapa kusoma na hivyo basi itakuwa inachangia kuboresha hali ya elimu katika eneo hili,” akasema.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Bw Samuel Kazungu alisema kuwa shule hiyo ambayo imeanzia katika masomo ya chekechea ina jumla ya wanafunzi 150.

“Tumeanzia daraja la kwanza, la pili, hadi darasa la tatu kwa sasa. Hii shule imekuwa na shida nyingi lakini mwezi wa Mei, tulipata wafadhili kupitia kwa mbunge wetu.

Tulikuwa na mkutano mkubwa hapa na watu walijaa. Baada ya huo mkutano tukaahidiwa kwamba shule itajengwa. Tunashukuru kufikia sasa, kazi inaendelea,” akasema Bw Kazungu.

Aidha alisema kuwa pindi tu shule hiyo ikikamilika, viwango vya elimu katika siku zijazo itaimarika.

“Tunajengewa madarasa manne na kufikia mwaka ujao, tutakuwa na wanafunzi wa darasa la nne. Haya ni mambo ambayo yanatutia moyo sana kwa sababu yana lengo la boresha elimu yetu,” akasema.

Mzee wa mtaa wa eneo la Zia Ra Wimbi Bw Kenga Karisa alisema kuwa walijaribu sana miaka ya nyuma kupata mshika dau ambaye angesaidia shule bila mafanikio.

“Baada ya kukosa matumaini tuliamua tu kama wakazi tuendelee pole pole kutatufa njia ya kujenga majengo ya udongo.

Mwaka huu mwezi wa Mei, ndipo mbunge alifika hapa na kumleta mfadhili ambaye aliamua kujenga shule hii. Vijiji ambavyo vitanufaika na ujenzi huu ni kama vile Zia Ra Wimbi A, Zia Ra Wimbi B, Kapangani na Mpungulu,” akasema.

Akiongea na wanahabari katika eneo kunakoendelea ujenzi huo, Bw Mwambire alisema kuwa ujenzi huo unafadhiliwa na ubalozi huo kwa kitita cha Sh12 milioni.

“Nilienda kuomba msaada kwa ubalozi huo kwa sababu ninajua changamoto ambazo ziko katika kijiji hiki. Watoto wanasomea katika mazingira magumu tena chini bila madawati,” akasema Bw Mwambire.

Mbunge huyo alisema kuwa shule hiyo ilianzishwa zamani lakini hakuna maendeleo yoyote ambayo yalikuwa yamepatikana.

“Tumejaribu kuangalia ni njia gani nzuri ya kuboresha elimu yetu katika Ganze. Kwanza ni kuboresha miundo msingi katika shule zetu,” akasema Bw Mwambire.