HabariSiasa

Raila atakuwa debeni 2022 – Orengo

August 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, anajiandaa kuwania tena urais mwaka 2022, washirika wake wa kisiasa wamefichua.

Wandani watatu wakuu wa Bw Odinga akiwemo Seneta wa Siaya James Orengo, walisema hakuna sheria yoyote inayomzuia Bw Odinga kuwania urais na hivyo, ana kila nia ya kushiriki kinyanganyiro kijacho cha kuwania urais.

Tangu Bw Odinga alipoweka makubaliano na Rais Uhuru Kenyatta, amekuwa akiepuka kuzungumzia maazimio yake ya kuongoza taifa hili na badala yake kusisitiza kwamba lengo lake kuu ni kuleta umoja wa taifa.

Amekuwa pia akisuta wanasiasa wanaojipigia debe kwa uchaguzi huo wa kumrithi Rais Kenyatta, hali ambayo iliacha wafuasi wake wengi kujiuliza kama ameamua kustaafu baada ya kujaribu kuwa rais mara nne na kushindwa, wakati mwingine katika hali tatanishi.

Kulingana na Bw Orengo, kwa sasa waziri huyo mkuu wa zamani ameweka mawazo yake katika juhudi za kupatanisha taifa lakini juhudi hizo ni miongoni mwa mikakati ambayo itamwezesha kufanikisha maazimio yake.

“Kabla wana wa Israeli kufika Kanani, iliwabidi wapitie Sinai kupokea Amri Kumi ambazo zingewaongoza na hilo ndilo tunajaribu kufanikisha. Lazima tuwe na mwongozo wa kimsingi ndipo Kenya izidi kuwa na amani na ipate heshima ulimwenguni kite. Tunataka nchi ambapo viongozi watakuwa wakiadhibiwa wanapokosea,” akasema Bw Orengo.

Alikuwa akizungumza katika Shule ya Upili ya Imbale, iliyo Kaunti Ndogo ya Ikolomani wakati wa mazishi ya Bi Bilha Akatsa ambaye ni mama mkwe wa Mbunge wa zamani wa Gem, Bw Joe Donde.

Chama cha ODM kina viongozi wengine wanaomezea mate tikiti ya kuwania urais 2022 wakiwemo Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya na inasubiriwa kuonekana kama wataingia naye kwenye mchujo wakati huo utakapofika.

Zaidi ya hayo, vinara wenza katika Muungano wa NASA ambao ni Kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) wamekuwa wakimtaka Bw Odinga kumuunga mkono mmoja wao ifikapo 2022.

Akizungumzia suala hilo, Mbunge katika Bunge la Afrika Mashariki, Bw Oburu Oginga, alisema Bw Odinga, ambaye ni kakake mdogo, hajakamilisha malengo yake kwa taifa hili.

“Watu wa ODM wasimame imara na waache kupayukapayuka kwa sababu Raila bado yuko,” akasema.

Msimamo huu uliungwa mkono na Gavana wa Siaya, Bw Cornel Rasanga, ambaye aliongeza kuwa Bw Odinga hajastaafu kutoka kwa siasa na hatachoka hadi Kenya itakapopata uongozi bora unaojali masilahi ya wananchi.

Kulingana na viongozi hao, ODM inaendelea kufanyiwa mageuzi ambayo yataimarisha uwezo wake zaidi na vilevile, kuna juhudi za kumfanya Bw Odinga kuwa na sura mpya kabla uchaguzi ufanywe.

Katika chaguzi zilizopita, wapinzani wa ODM walitangaza chama hicho kama kinachopenda fujo huku Bw Odinga akikashifiwa kuwa kiongozi asiyependa maendeleo na mwenye uwezo wa kugawanya nchi kikabila.

Lakini tangu alipoanza kushirikiana na Rais Kenyatta, kiongozi huyo wa upinzani ameanza kuonyesha mwelekeo mpya wa kisiasa ambao umemzolea sifa hata katika maeneo ambako ilikuwa vigumu kwake kupenya kufanya kampeni katika miaka iliyotangulia.